Mkakati bora wa kisiasa ni kuondoa vizingiti vilivyopo serikali za mitaa

Muktasari:

  • Serikali za mitaa ni vyombo vya wananchi ambavyo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania huundwa, huendeshwa na huwajibika kwa wananchi. Madhumuni ya kuwapo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.
  • Hii ni kwa kuwa wananchi ndio chimbuko la mamlaka yote katika nchi yetu, hivyo haitakiwi kuwapo vikwazo vya aina yoyote katika kufanikisha lengo hilo.
  • Tofauti na zile Serikali za mitaa zilizoanzishwa na ukoloni, Katiba ya Tanzania inaelekeza pia kwamba vyombo vya Serikali za mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma sehemu zao na chini kote kwa ujumla.

Kama tulivyoona katika makala zilizotangulia, Serikali za mitaa ni vyombo vya wananchi ambavyo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania huundwa, huendeshwa na huwajibika kwa wananchi. Madhumuni ya kuwapo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.

Hii ni kwa kuwa wananchi ndio chimbuko la mamlaka yote katika nchi yetu, hivyo haitakiwi kuwapo vikwazo vya aina yoyote katika kufanikisha lengo hilo.

Tofauti na zile Serikali za mitaa zilizoanzishwa na ukoloni, Katiba ya Tanzania inaelekeza pia kwamba vyombo vya Serikali za mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma sehemu zao na chini kote kwa ujumla.

Serikali za mitaa nchini zilikuwepo hata kabla ya wakoloni hawajaitawala nchi hii. Utawala wa Mjerumani haukutambua Serikali za wenyeji na badala yake ukaweka mawakala wake.

Utawala huu wa Mjerumani ulikuwa wa nguvu na ndiyo maana wananchi walianzisha vita ili kupambana nao. Kwa upande wake Utawala wa Mwingereza ulitambua Utawala wa wenyeji na ukauhalalisha kwa Sheria Na.72 ya mwaka 1926. Vilevile, utawala wa Mwingereza ulitunga sheria Na.333 ya mwaka 1953 katika jitihada zake za kuendeleza mfumo wa Serikali za Mitaa nchini. Dosari kubwa inayojitokeza katika Serikali za Mitaa zilizoundwa ni kwamba, wajumbe walioingia katika mabaraza hayo moja kwa moja hawakuwawakilisha wananchi.

Hivyo, demokrasia ya kweli haikuwapo. Jambo hili lilirekebishwa na Serikali ya wananchi mara baada ya uhuru ikiwa ni pamoja kufutwa kwa utawala wa machifu mwaka 1963.

Kutokana na matatizo yaliyozikumba Serikali za Mitaa ya kukosa fedha, watumishi na ubadhirifu zilifutwa mwaka 1972 na badala yake ulianzishwa mfumo wa madaraka mikoani.

Hata hivyo, utaratibu huu wa madaraka mikoani ulidumu kwa karibu miaka kumi tu, ambapo mwaka 1982 Serikali za mitaa, ziliporejeshwa tena baada ya kudhihirika umuhimu wa Serikali za Mitaa, kisha uliingizwa katika Katiba ya mwa 1977 na sheria Na. 7 na 8 za mwaka 1982 za Bunge na hivyo kuhalalisha kuwepo kwake.

Kuanzia miaka ya 1990 na kuendelea, harakati mbalimbali zilifanyika ili kuziboresha Serikali za Mitaa nchini. Uboreshaji wenyewe ulianza rasmi mwaka 2000. Taifa letu linaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo si kwa ushindani wa vyama vya siasa na majigambo ya vyama vya siasa, na wala si kwa ushindi wa kishindo, au kwa tumbuatumbua na utekelezaji wa mapenzi ya mtu moja mmoja, bali ni kwa kufuata siasa za kimkakati.

Na mkakati mmoja wapo ambao ndiyo msingi wa maendeleo ya mataifa makubwa duniani ni uboreshaji wa serikali za mitaa. Tukifanikiwa kulifanya hili, ambalo kwa hekima na busara linaweza kufanikishwa kwa ushirikiano wa vyama vyote vya siasa, vyama vya kijamii na vya kidini hata na watu ambao hawana vyama.

Pamoja na maboresho hayo ya serikali za mitaa bado kuna vizingiti vikubwa vya uboreshaji huu ambavyo ni: ubadhirifu, rushwa, unyanyasaji wa wananchi, huduma duni, kutojali sheria na taratibu zilizowekwa, kutowajibika, kutowashirikisha wananchi.

Ubadhirifu

Kumekuwepo na malalamiko mengi ambayo yamethibitishwa na taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu matumizi mabaya ya fedha, watumishi na mali za Halmashauri. Mara nyingi ubadhirifu huu umetokana na maamuzi mabaya ya na mara nyingine kutokana na kutojali kwa watumishi wa halmashauri.

Matokeo ya ubadhirifu huu yamekuwa yakidhoofisha halmashauri husika; kudorora kwa huduma muhimu kwa wananchi na kupoteza imani ya wananchi kwa Serikali yao, na hivyo kususia wajibu wao wa kulipa kodi na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii. Hivyo kule tunakokwenda katika mfumo huu wa Serikali za mitaa, ni muhimu kupambana na ubadhirifu kwa nguvu zote, ili kuleta ufanisi zaidi katika maendeleo ya taifa letu.

Rushwa

Si jambo la siri kuwa rushwa imetanda na kukithiri katika halmashauri zetu, hasa katika masuala yanaohusu utoaji wa huduma muhimu kama tiba, elimu, leseni za biashara, ugawaji wa viwanja, utoaji wa zabuni na ajira za watumishi. Vitendo vya rushwa vinafanyika wazi bila aibu, na vinachukuliwa kama vitendo vya kawaida vinavyoendana na wakati. Pamoja na msimamo mkali wa Rais Magufuli, pamoja na tumbua tumbua, bado rushwa iko palepale. Matokeo yake ni wananchi kunyimwa haki zao za kimsingi, na kupoteza imani na hata huichukia Serikali yao.

Kwa baadhi ya viongozi wetu uongozi umegeuzwa kuwa biashara na si utumishi wa umma. Rushwa imechukuliwa kama kichocheo muhimu cha kujiimarisha kabla muda wa kuachia ngazi haijawadia. Hivyo kule tunakokwenda katika mfumo huu wa Serikali za mitaa, ni muhimu kupambana na rushwa kwa nguvu zote, ili kuleta ufanisi zaidi katika maendeleo ya taifa.

Unyanyasaji wa wananchi

Baadhi ya viongozi katika halmashauri wamepoteza dira ya uongozi, badala yake wamekuwa wakitumia nafasi zao kuwakandamiza na kuwanyanyasa wananchi. Vitendo hivi vinajitokeza waziwazi katika baadhi ya mbinu zinazotumika katika ukusanyaji wa kodi na aina nyingine za mapato, na pia katika utekelezaji wa sheria ndogondogo za halmashauri. Vyombo vya habari vimeonyesha mara nyingi jinsi wafanyabiashara, na hasa wanaosafirisha bidhaa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine wanavyopata wakati mgumu kupambana na watoza ushuru katika halmashauri mbalimbali. Hali hii ni muhimu kupambana nayo kwa nguvu zote.

Huduma duni

Kero nyingine ni ile inayohusu huduma duni zinazotolewa kwa wananchi kutokana na uzembe na kutojali kwa viongozi na watendaji. Licha ya kutambua hali ngumu ya kiuchumi na upungufu wa mapato, wananchi wanategemea viongozi wao kuhakikisha kuwa rasilimali iliyopo inatumika kikamilifu katika utoaji wa huduma za jamii katika kuweka miundombinu itakayowawezesha kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na maendeleo. Mara nyingi huduma muhimu na miundombinu vimeachwa kudorora, na hata kuharibika kabisa, hadi serikali kuu inapoingilia katikati na kuwachukulia hatua wahusika kwa kutowajibika ipasavyo. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha huduma muhimu zinatolewa ipasavyo ili kuleta ufanisi zaidi.

Kutojali sheria, taratibu

Sheria na taratibu mbalimbali zimewekwa ili kuongoza shughuli za halmashauri zetu; kulinda haki za msingi za wananchi na kudhibiti vitendo visivyotakiwa au kukubalika katika jamii. Licha ya ukweli huo, umezuka mtindo ambamo baadhi ya viongozi na watumishi katika halmashauri hawajali sheria wala taratibu zilizopo.

Suala la sheria ni muhimu sana, la sivyo ni vigumu kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi. Sheria inakuwepo kulinda haki ya wananchi wote, bila kuangalia sura, dini, kabila au uwezo wa mtu. Kuna mifano mingi kuhusu jambo hili: kuvuruga kwa makusudi mipango ya matumizi ya ardhi katika sehemu za miji; kuruhusu biashara kuendeshwa kiholela, kutumia fedha bila kujali taratibu na kanuni za fedha na mengine.

Mtindo unaoonekana kupendwa sana na baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali, ni ule wa kutoa maagizo ya mara kwa mara kutaka hili au lile lifanyike katika muda wanaoutaka bila kujihakikishia kwanza kama sheria na taratibu zilizopo zinaruhusu na kama maagizo hayo yana maslahi kwa wananchi.

Sheria na utaratibu vinasaidia kufuata mapenzi na matakwa ya wananchi zaidi ya kufuata mapenzi na matakwa ya mtu binafsi. Sasa hivi kila mwenye madaraka anatoa maagizo, bila kurejea kwanza kwenye sheria zilizopo. Hivyo kule tunakokwenda katika mfumo huu, ni muhimu kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.

Kutowajibika

Suala la uwajibikaji limekuwa linazungumzwa zaidi kuliko kutekelezwa. Fikra zilizotanda kwa walio wengi ni kwamba wanaopaswa kuwajibika kutokana na matokeo ya utendaji wao ni watumishi peke yao. Utaratibu wa viongozi kutoka taarifa kwa wapiga kura wao kuhusu utendaji wao ni jambo la nadra, na kwa wengi halipo kabisa. Pia si jambo la kawaida kuona kiongozi kwa hiari yake anakubali kuwajibika kwa maamuzi yake ambayo yameleta madhara makubwa kwa wananchi.

Kinachoonekana zaidi ni utetezi usio na mwisho wala msingi pindi wananchi wanapoamua kuchukua hatua. katika mfumo huu wa Serikali za mitaa, ni muhimu kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa kwa ngazi zote za uongozi kupambana na ubadhirifu.

Kutowashirikisha wananchi

Maamuzi mengi yanafanywa na halmashauri na kuwaathiri wananchi moja kwa moja bila kwanza kupata maoni yao. Tumeendeleza mno utawala msonge ambapo viongozi wamegeuka kuwa mabwana wenye kutoa amri na kufuatilia utekelezaji wake kwa nguvu zote. Kwa upande mwingine, halmashauri zimeendelea kubeba jukumu lote la utoaji wa hudumu muhimu, na pia kubuni na kutekeleza mipango yote ya maendeleo katika sehemu zao. Wananchi wamebaki kuwa watazamaji tu wa huduma zinazotolewa, hali ambayo imewadumaza na hivyo kuchelewesha maendeleo yao wakati wakingoja halmashauri ziwafanyie kila kitu.

Matokeo ya kutowashirikisha wananchi katika masuala yanayohusu ustawi na maendeleo yao, ni kuongezeka kwa malalamiko yao na kurudisha nyuma jitihada ya kuwa na maendeleo endelevu.

Niliyoyaorodhesha hapo juu yakifanyiwa kazi na kuboreshwa, tutafanikiwa kuwa na serikali za mitaa zenye nguvu na zenye kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Tukiwa na serikali za mitaa zenye ufanisi, ni wazi tutafanikiwa kulijenga taifa lenye mshikamano na maendeleo. Hapa kazi tu, iwe kweli Hapa kazi tu! Si matamko tu bali ni kuyafanyia kazi matamko hayo!

Padre Privatus Karugendo.

+255 754633122