Tutumie 2020 – 2025 kujenga mifumo imara

Sunday September 16 2018Julius Mtatiro

Julius Mtatiro 

By Julius Mtatiro

Ni wazi kuwa yako masuala makubwa ambayo yamefanywa na yanaendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Tunayazungumza sana masuala hayo kwa sababu ni mambo makubwa kwa asili na utendekaji wake.

Natambua kuwa kumekuwa na mjadala wa muda mrefu wa uhusiano wa masuala hayo na hali halisi ya maendeleo ya kawaida ya Mtanzania wa kawaida, mjadala huo unaweza kuendelea, nami siku za mbele nitaandika kuhusu uhusiano huo.

Fikra zangu za leo zinajikita kwenye utunzaji wa masuala hayo makubwa yanayotendwa na Serikali ya awamu hii. Jumapili iliyopita nilizungumza kidogo kuhusu dhana ya mambo hayo makuu na namna yatakavyodumishwa siku za usoni, nikaonesha matamanio yangu kuwa mambo hayo yanapaswa kujengewa msingi na uzio ili yaendelezwe kimfumo na kitaasisi hata siku JPM akiwa hayupo madarakani.

Fikra zangu hizo zimekuja kwa sababu sote ni wenyeji wazuri wa siasa za Afrika ambapo uongozi mmoja unapoondoka madarakani, upo uwezekano mkubwa uongozi unaofuatia ukaacha kutilia mkazo kwenye masuala makubwa na muhimu na yenye tija ambayo huwa yametendwa na uongozi uliopita.

Hali hii hutokea kwenye mataifa mengi na athari zake huwa ni kubwa. Kwa hiyo, Afrika isipochukua hatua kwenye eneo hili na hasa Tanzania, tutaingia kwenye matatizo makubwa ambayo tumewahi kuyapitia.

Kipindi cha 2015 – 2020

Wakati Serikali ya JPM ikiwa na miaka miwili na nusu madarakani, miradi mkubwa ya maendeleo imekwishatekelezwa, hapa nazungumzia ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania, ujenzi wa mradi wa Umeme wa stiegler’s Gorge, ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga na mambo mengine mengi.

Katika kipindi hiki cha miaka miwili na nusu tunashuhudia pia kukiwa na mabadiliko makubwa kwenye vita ya rushwa na ufisadi, nidhamu ya watendaji serikalini, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na mitandao ya wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo, viongozi wa Serikali wakitumia muda mwingi kutatua shida za wananchi kwenye maeneo ya wananchi kuliko kukaa maofisini na hatua zingine.

Yako mengi yanayofanyika na yamesemwa na watu wengi kila wanapojiweka kwenye nafasi ya katikati. Na ni kawaida masuala hayohayo yakafanywa madogo kila yanapotathminiwa na mtu aliye na upande maalumu kwenye tafakari hiyo. Mimi mwenyewe, nimewahi kushiriki kwa kina kwenye tafakari hizo.

Kukiri maendeleo

Lakini, hata wakati tukiwa upinzani bado wapo viongozi wamethubutu kuelezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano.

Mathalani, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alijiweka kwenye upande huu wa kukumbuka kwamba yako masuala yanafanywa vizuri katika Serikali ya sasa, Julai 22, 2017 wakati akimpokea Rais Magufuli Kigoma, alimweleza “...watu wa Kigoma wanataka maendeleo, na wewe (Rais Magufuli) unatuletea maendeleo, ndiyo maana (watu wa Kigoma) wanakupenda...”

Maneno haya ya kiongozi wa juu kabisa wa upinzani ni ushahidi kuwa huko upinzani kwenyewe tulikuwa tukikiri kimyakimya au hadharani kuwa yako mambo makubwa yanafanywa na Serikali ya awamu hii, makubwa kushinda tulivyokuwa tunatarajia.

Fedha za maendeleo

Mei 2, 2018, Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema, Mchungaji Peter Msigwa alipopewa nafasi ya kuzungumza mbele ya JPM ikulu ndogo huko Iringa, alieleza;

“Mhe. Rais umekuwa ukisisitiza katika hotuba zako kuwa wewe hujali mambo ya vyama, na hii imedhihirika kuwa kweli hujali vyama, umesaidia sana, hela za kutoka kwako zimekuja nyingi. Kama alivyosema Mhe. Mahiga, kuna barabara nzuri katika kipindi chako ambacho umekuwa Rais, umejenga barabara ya lami kutoka Mlandege mpaka kwa Mkuu wa Wilaya karibu Sh3.5 bilioni.

Msigwa akaendelea, “Tuna stendi nzuri ipo Ipogolo ya karibu Sh 3 bilioni, tuna maji, kwa hiyo kuna vitu vimefanyika kwa kweli Mhe. Rais hupendelei, hela zinakuja hata sisi ambao ni wa Chadema unaleta hela, kwa hiyo tunakupongeza sana.”

Maneno haya ni ushahidi mwingine kuwa pamoja na malalamiko ya masuala mbalimbali ambayo wamekuwa nayo viongozi wa vyama vya upinzani dhidi ya Serikali, jambo moja kubwa ambalo wanakiri ni kuwa, Rais Magufuli anapigania maendeleo ya taifa hili na anayapigania kufa na kupona na hana mchezo kwenye maendeleo.

Kwa kipindi kirefu taifa letu lilikuwa linalia, linamlilia kiongozi ambaye angeliweza kututoa kwenye matumizi mabaya ya fedha na kukosa vipaumbele vya maendeleo, Mungu akatujalia na kutuletea mtu ambaye kwake maendeleo ni kama maji, anayataka na anayapigania usiku na mchana – isingelikuwa rahisi sana kwa viongozi wakubwa wa upinzani kuficha hisia zao dhidi ya mtu wa aina hiyo.

Ndiyo, mtu wa aina hiyo anaweza kuwa na mapungufu yake na anaweza kuwa hafanyi vizuri sana kwenye baadhi ya maeneo mengine, lakini tayari anafanya vizuri kwenye eneo kubwa kuliko yote kwa Watanzania – maendeleo. Ukifanya utafiti wa wazi na ukawauliza Watanzania wote nchi nzima, nini kipaumbele chao nambari moja watakwambia wanataka maendeleo kwa vitendo, wanataka amani.

Msimamizi wa maendeleo

Rais JPM amekuwa msimamizi mkubwa wa maendeleo hayo na anatumia fedha nyingi za umma kuleta maendeleo, wala si kuzila pesa hizo yeye au kujishibisha yeye na familia yake. Kasi hiyo ya JPM imewahi kuthibitishwa na aliyekuwa mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa alipokwenda kumtembelea Ikulu, viongozi wakubwa wa dini wakiwamo wale wa TEC ambao walikwenda kumtembelea Rais mwaka huu 2018.

Nilipokuwa kiongozi wa juu wa upinzani na hata mwenyekiti mwenza wa Ukawa, ilitupasa sisi viongozi wa juu mara kwa mara kujitokeza hadharani kupangua hoja za aidha wabunge wetu au viongozi wenzetu wa upinzani waliojitokeza hadharani na kukiri kuwa awamu hii ni ya maendeleo.

Mimi mwenyewe nilisimama hadharani na kuwazodoa wabunge au viongozi hao. Lakini, ningelifanya hivyo hadi lini? Ningeendelea kujificha chini ya falsafa ya kutetea ajenda za upinzani zilizoporwa na JPM hadi lini? Isingeliwezekana hasa kwa kuzingatia kuwa tayari chama changu kimekuwa kwenye matatizo makubwa sana ambayo hata yakiisha salama kitakuwa kimeshafutika upande wa Tanzania Bara.

Na kwa sababu ajenda yangu kubwa katika maisha yangu imekuwa ni kupambana na umasikini na rushwa na ufisadi, isingelikuwa rahisi kuendelea kujificha kwenye mwamvuli wa kupinga hatua zinazofanywa na Serikali kupambana na umasikini na rushwa na ufisadi.

Na huenda wako viongozi wengi wakubwa ambao wanaridhika kuwa utendaji wa sasa wa Serikali unapaswa kuungwa mkono, na kasi ya utendaji wa Serikali inapaswa kutangazwa hivyo ilivyo maana mwisho wa siku maendeleo yanayotendwa hivi sasa yanafanywa kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali vyama vyao, rangi zao, kabila zao na sababu nyinginezo.

Hata nisingekiri, mawe yangezungumza Kama jambo kubwa na zuri linafanyika mahali na nyinyi hamlikiri, hata mawe yatazungumza. Hata kama nisingelijitokeza na kuachana na siasa za kupinga na kuzodoa na kuanza kujihusisha na siasa za maendeleo na kuboresha kwenye maendeleo, wapo wengi wangelijitokeza na kukiri.

Hata kabla sijakiri kuwa awamu hii ya Serikali ya tano inafanya kazi kubwa ya maendeleo ambayo ni ajenda kubwa ya Watanzania, tayari kaka zangu Zitto Kabwe, Peter Msigwa na Edward Lowassa walisimama hadharani wakafanya hivyo, hawakufanya kwa niaba ya vyama vya upinzani bali kwa nafsi zao wenyewe.

Matamanio ya viongozi wengi wa CCM na upinzani ya kuijenga Tanzania yenye maendeleo yatakuwa hayana maana ikiwa mikakati ya sasa ya JPM ya kulikimbiza taifa mbele haitajengewa mifumo imara ya kuendeleza masuala muhimu ya kiutendaji na kiusimamizi hata JPM atakapotoka madarakani.

Jumapili ijayo nitajadili sehemu ya mwisho ya makala hii kwa kina, ambapo nitajikita kwenye mbinu na mikakati muhimu tunayoweza kuifanya kati ya 2020 – 2025 ili mikakati ya uletaji wa maendeleo chini ya JPM iwe ni suala la kudumu na la kimfumo ili hata atakapoondoka madarakani.

Julius Mtatiro ni mtafiti na mchambuzi wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mwanasheria, mfasiri na mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera. Barua Pepe; [email protected])

Advertisement