Uvimbe na kutokwa damu kwenye njia ya haja kubwa

Muktasari:

Hili ni tatizo la kiafya kitaalamu linaitwa ‘Hemorrhoids’.cha kusikitisha ni kwamba, wagonjwa wengi hawapati tiba sahihi inayostahili kwa kuwa wanaona aibu kuwaona watoa huduma wa afya kwa ajili ya ushauri na tiba sahihi ya namna ya kulimaliza tatizo hilo.

Unaweza kuhisi una uvimbe mdogo sehemu ya nje ya njia ya haja kubwa inayoambatana na muwasho na maumivu makali. Wakati mwingine ukienda haja, unajisaidia kwa shida kwa kutumia nguvu kubwa kusukuma na hata kinyesi kikitoka kinakuwa kimechanganyika na damu.

Hili ni tatizo la kiafya kitaalamu linaitwa ‘Hemorrhoids’.

cha kusikitisha ni kwamba, wagonjwa wengi hawapati tiba sahihi inayostahili kwa kuwa wanaona aibu kuwaona watoa huduma wa afya kwa ajili ya ushauri na tiba sahihi ya namna ya kulimaliza tatizo hilo.

Wengi huamua kwenda kwenye maduka kununua dawa bila ushauri wa daktari kwa matumaini ya kulikabili tatizo. Ni vema kutambua ukweli kwamba, kutokwa na damu sehemu za siri kunahitaji msaada zaidi wa daktari ili kubaini tatizo. Wajawazito wanakua hatarini zaidi kupata tatizo hili. kadiri mimba inavyozidi kukua, mwanamke hupata mabadiliko mbalimbali ya kimaumbile likiwamo la mfuko wa uzazi kupanuka na kuongezeka uzito kunakosababisha mkandamizo kwenye utumbo mpana.

Kadhalika, wazee pia hupata tatizo hilo kutokana na mfumo wa kinga yao ya mwili kufifia kunakosababishwa na umri. Tofauti na wajawazito na wazee, kundi lingine ambalo lipo hatarini ni la wale wanaofanya ngono kinyume na maumbile. Lakini tusisahau kuwa tatizo hili linaweza kumpata mtu yeyote. Mtu anapopatwa na tatizo hili, mara nyingi kwenye sehemu ya ndani ya ngozi ya njia ya haja kubwa huvimba na kutokeza nje.

Tatizo hili linatibika kama mgonjwa atapata msaada wa kitabibu mapema, hivyo mgonjwa anashauriwa kumuona daktari haraka mara tu agunduapo dalili za awali ikiwamo ya kutokwa na damu kusikoambatana na maumivu au maumivu ya kawaida, muwasho ndani na nje ya sehemu ya haja kubwa, maumivu kwenye sehemu ya haja kubwa hasa wakati ukiwa umekaa, kuhisi uvimbe sehemu ya haja kubwa na kuhisi sehemu ya ndani ya haja kubwa imetokeza nje. Mtu yeyote anayepitia dalili hizi anapaswa kumuona daktari haraka.

Ni vema ikafahamika kuwa, baadhi ya matatizo makubwa ya kiafya kama ya saratani ya utumbo na saratani ya njia ya haja kubwa zinasababisha utokaji damu sehemu ya haja kubwa. Ni kosa kubwa kudhani kuwa kutokwa na damu kwenye njia ya haja kubwa ni tatizo la kawaida hivyo mtu akaamua kupuuzia kupata ushauri wa daktari.

Wakati mwingine mgonjwa hulazimika kufanyiwa upasuaji mdogo iwapo anakua amechelewa kupata tiba kwa muda sahihi.

Tatizo hili linatokea wakati ambapo mishipa midogo midogo kwenye njia ya haja kubwa hutanuka na kusababisha ngozi ya sehemu ya ndani ya haja kubwa kutokeza nje kutokana na maambukizi mbalimbali.

Tatizo hili mara nyingi husababishwa na maambukizi ya vimelea vya maradhi ambavyo aidha yameanzia ndani kwenye utumbo mpana wa chakula au sehemu ya haja kubwa.

Sababu nyingine kubwa zinasababisha tatizo hilo ni mwili kukosa kiwango stahiki cha maji. Mwili unahitaji kiasi cha kutosha cha maji ili chakula kiweze kumeng’enywa vizuri tumboni, hivyo upungufu wa maji mwilini unaweza kuathiri mmeng’enyo wa chakula na hivyo kusababisha mtu kutoa kinyesi kigumu.

Kutokana na ugumu huo, kinasababisha michubuko kwenye njia ya haja kubwa wakati wa kutoka na michubuko hiyo inaweza kusababisha maambukizi.

Ulaji wa mboga za majani na matunda kwa wingi unasaidia kukabiliana na tatizo hili kutokana na nyuzi lishe zinazopatikana kwenye kundi hilo la vyakula.

Njia sahihi ya kukabiliana na tatizo hilo ni kwa jamii kujenga utamaduni wa kunywa maji ya kutosha, kufanya mazoezi na kula matunda yenye nyuzi lishe kwa wingi, mboga za majani na vyakula visivyokobolewa, kwa sababu vitu vyote hivyo kwa pamoja vinasaidia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula mwilini na kukifanya kinyesi kiwe kilaini na kitokapo hakiwezi kusababisha msuguano unaoanzia ndani kwenye utumbo mpana hadi sehemu ya haja kubwa.