Makandarasi, Tanroads watuhumiana

Muktasari:

Aliwataka wanaoamini hawakutendewa haki au kudaiwa rushwa katika mchakato wa zabuni, wakatoe taarifa ofisini kwake.

Moshi. Kutokana na tuhuma za makandarasi mkoani Kilimanjaro kulalamikia upendeleo wa zabuni kwa baadhi ya kampuni, Meneja wa Tanroads Mkoa wa huo, Ntije Nkolante amesema hawezi kuzizungumzia akisisitiza utoaji zabuni unazingatia sheria.

Aliwataka wanaoamini hawakutendewa haki au kudaiwa rushwa katika mchakato wa zabuni, wakatoe taarifa ofisini kwake.

Baadhi ya makandarasi walilalamikia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro, kwa kutoa zabuni kwa upendeleo kwa baadhi ya kampuni walizodai hazina uwezo.

Makandarasi hao walienda mbali na kumtuhumu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi (PMU), Reginald Massawe kwa madai ya kuzipendelea kampuni walizodai kuwa ana masilahi binafsi.

Hata hivyo, Massawe alikanusha kumiliki kampuni ya ujenzi ambayo imekuwa ikipata zabuni ndani ya Tanroads kama inavyodaiwa na baadhi ya makandarasi.

 Pia, Massawe alikanusha madai ya makandarasi hao kuwa amekuwa akiingilia na kubatilisha mapendekezo ya bodi ya uthamini na kuzipa kazi kampuni ambazo ana maslahi nazo.

Baadhi ya makandarasi walidai kuwa Tanroads inatakiwa kutangaza upya zabuni ya ujenzi wa madaraja ya Kia na Kifaru, kwa sababu aliyepewa ameshindwa kazi.  

Kampuni hiyo ambayo jina tunalo, inadaiwa kuonyesha ingejenga madaraja hayo kwa Sh260 milioni, wakati uhalisia kazi hiyo ni zaidi ya Sh500 milioni.