Makonda kuwakamata waliotelekeza watoto Jumatatu

Muktasari:

Makonda amesema akishirikiana Kamanda Lazaro Mambosasa wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu  ya Dar es Salaam, watawakamata wanaume wote waliokaidi wito huo


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema wanaume waliopokea barua za kuitwa ofisini kwake kwa ajili ya maridhiano na wazazi wenzao na wakakaidi, ifikapo Jumatatu watakamatwa kwa mujibu wa sheria. 

Akizungumza leo Aprili 20 wakati wa kuhitimisha zoezi hilo la siku 10, Makonda amesema akishirikiana na Kamanda Lazaro Mambosasa wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, watawakamata wanaume wote waliokaidi wito huo. 

“Kwenye utawala huu wa awamu ya tano kila mtu atawajibika kwa nafasi yake, leo ni siku ya 10 kwa mwanaume yeyote ambaye amepigiwa simu, ametumiwa barua halafu amekaidi wito kuanzia Jumatatu ninawakamata wanaume waliokimbia majukumu yao,” amesema Makonda.

Amesema alipotangaza Machi 8 akasema zoezi litaanza Aprili 9 alitoa mwezi mzima kwa watu walio na busara warekebishe mambo yao  na akasema kuwa wapo waliotekeleza agizo hilo lakini wengi walikaidi.

Amesema hawezi kuongoza mkoa ambao unaendelea kuwa na watoto ombaomba wakati baba zao wapo.

Hata hivyo, awali zoezi hilo lilikuwa la siku 10 lakini Mkuu huyo wa Mkoa, ameongeza siku tano nyingine.