Makunga aeleza sababu kujiuzulu kwake uongozi TEF

Muktasari:

  • Makunga aliandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Ijumaa (Machi 16, 2018) kabla ya kuutangaza jana kwa wajumbe wa jukwaa hilo waliokutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa dharura ambao ulikubaliana na uamuzi huo.

Baada ya mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo, nguli huyo amesema sababu ya uamuzi huo ni kupumzika ili kupata muda wa kufanya shughuli nyingine za ushauri wa kitaaluma.

Makunga aliandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Ijumaa (Machi 16, 2018) kabla ya kuutangaza jana kwa wajumbe wa jukwaa hilo waliokutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa dharura ambao ulikubaliana na uamuzi huo.

Hata hivyo, uamuzi wa Makunga kujiuzulu umehusishwa na tukio la kwenda katika hafla ya kampuni moja ya magazeti na kulishika kama njia ya kulitangaza wakati likidaiwa kuandika habari zisizozingatia maadili ya uandishi wa habari, suala lilioibua mjadala miongoni mwa wanahabari nchini.

Makunga aliliambia Mwananchi kuwa hakuna uhusiano wa kujiuzulu kwake na uamuzi wa kushiriki sherehe za kutimia mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa gazeti hilo. Aisema hakuna kanuni katika jukwaa hilo inayomzuia kutembelea gazeti lolote.

“Nimejiuzulu ili nipumzike nafasi hiyo, nipate nafasi ya kufanya kazi nyingine za ushauri, ninayo kampuni ya ushauri inaitwa Mabadiliko Communications Limited, lakini bado nitaendelea kushiriki jukwaa kama mwanachama wa kawaida,” alisema Makunga ambaye amewahi kuwa mhariri mtendaji wa Mwananchi.

Taarifa iliyotolewa jana na katibu mkuu wa jukwaa hilo, Neville Meena ilieleza kuwa Makunga amechukua uamuzi huo akitumia uhuru wake kama mwanachama hai.

“Makunga amechukua hatua hiyo kwa kutumia uhuru wake binafsi kama mwanachama hai wa TEF, Kutokana uamuzi huo, mkutano mkuu wa dharura wa TEF uliofanyika leo (jana) umeridhia kujiuzulu kwake,” ilinukuu sehemu ya taarifa ya TEF.

Meena alisema makamu mwenyekiti anachukua nafasi hiyo hadi mkutano mkuu utakapofanyika tena hapo baadaye mwaka huu, ambao utaamua kuchagua mwenyekiti mwingine au kuendelea kwa makamu mwenyekiti aliyekabidhiwa mikoba hiyo kwa sasa.

Makunga ameongoza TEF katika harakati mbalimbali ikiwamo kutoa matamko na kutetea uhuru wa vyombo vya habari tangu alipoingia madarakani Januari 2016 baada ya kupokea kijiti kutoka kwa Absalom Kibanda.

Taarifa ya TEF, ilieleza kuwa pamoja na uamuzi huo, haitaubeza uongozi uliotukuka katika jukwaa hilo chini ya Makunga. Taarifa hiyo inasema ni dhahiri TEF itazikosa busara za Makunga ambazo zilikuwa bado zinahitajika katika ujenzi wa tasnia ya kitaaluma.