Mambo nane yaliyoacha gumzo harusi ya Shilole

Muktasari:

Ndoa hiyo imekuwa gumzo kutokana na umaarufu alikuwa nao msanii huyo ikiwemo katika suala la mahusiano aliyowahi kupitia kabla ya kukutana na Uchebe.

Desemba 6, mwaka jana, msanii wa muziki wa kizazi kipya na filamu, Shilole alifunga ndoa na mpenzi wake Ashraf Uchebe.

Ndoa hiyo imekuwa gumzo kutokana na umaarufu alikuwa nao msanii huyo ikiwemo katika suala la mahusiano aliyowahi kupitia kabla ya kukutana na Uchebe.

Baada ya ndoa hiyo, Januari 15 mwaka huu, siku ya Jumapili walifanya sherehe ya kukata na shoka maeneo ya Mikocheni na kuhudhuriwa na masupastaa kibao ambapo huenda ikawa ni harusi ya kwanza kuwakutanisha wasanii wengi wa Bongo Fleva na Bongo Movie nchini.

Zawadi

Katika sherehe hiyo kulikuwa na mambo mbalimbali, lakini yapo ambayo yameacha historia hadi leo vichwani mwa watu ikiwemo zawadi ambazo hazijazoeleka kutolewa katika harusi hususani za wasanii.

Kama ni mfuatiliaji wa harusi za wasanii wengi, zawadi kubwa tunazoziona ni kutanzana fedha lakini kwa Shilole imekuwa tofauti kwani ameweza kupata zawadi ambazo zitamuinua kutoka hapo alipo na kwenda hatua nyingine.

Kutangaziwa bidhaa yake ya pilipili

Katika harusi hiyo pamoja na mambo mengine kubwa ni lile la msanii maarufu, Naseeb Abdul’Diamond’ alipoitwa kutoa zawadi yake na kumtaka Shilole achague zawadi anayoitaka kwa kuhofia kuna kitu ambacho angeweza kumpa kumbe anacho.

Pasipo kutegemea Shilole ambaye jina lake halisi ni Zuwena Mohammed alimuomba msanii huyo amtangazie bidhaa yake ya pilipili inayoitwa ‘Shishi Chili’ aliyoanza kuingiza sokoni hivi karibuni.

Anaomba hilo akijua wazi namna gani Diamond alivyo maarufu ndani na nje ya nchi na anavyofuatiliwa na watu wengi, hivyo kumsaidia kutangaza bidhaa yake hiyo ataweza kujikuta anapata soko.

Hata hivyo Diamond mbali na kukubali kumtangazia, alienda mbali zaidi na kuahidi kumtengenezea na tangazo katika studio yake ya Wasafi bure.

Akizungmza siku hiyo, Shilole anasema haitaji fedha kutoka kwa msanii huyo, kwani anajua kuwezeshwa kwa namna hiyo kutaweza kumfanya aje kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa.

Kusomeshewa mtoto

Zawadi nyingine iliyoacha historia kwa harusi ya mama huyo wa watoto wawili ni msanii wa Bongo Fleva, Jux anayetamba na wimbo Utaniua kuahidi kumsomeshea mtoto wake mmoja mwaka mzima na kumlipia gharama zozote zitakazohitajika shuleni.

Kwa kufanya hivyo ni wazi kwamba atampunguzia Shilole mzigo wa kumsomesha ndani ya mwaka huu na fedha aliyokuwa aitumie kwa ajili ya ada na matumizi mengine ataweza kufanyia mambo mengine.

Gari la kusambazia bidhaa zake

Msanii mwingine aliyevunja rekodi katika sherehe hiyo, ni Harmonize ambaye yeye alimtaka Shilole akachague gari aina ya Noah isiyozidi Sh9 milioni kwa ajili ya kumsaidia kusambaza bidhaa zake.

Kwani mbali na muziki, Shilole anamiliki mgahawa wa chakula uliopo maeneo ya Moroco Jijini Dar es Salaam unaoitwa Shishi Food na amekuwa pia akisambaza chakula katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye ofisi.

Pia, bidhaa yake ya pilipili inaweza kujikuta ikapata lifti kupitia gari hilo hasa pale anapohitajika kupeleka mzigo mkubwa mahali.

Vanessa amlipia ‘honeymoon’

Kutokana na kuwa mchakarikaji mzuri katika kusaka pesa, Shilole na mumewe baada ya sherehe hiyo ilielezwa kwamba walikuwa hawana mpango wa kwenda fungate na badala yake walipanga kesho yake kwenda mgahawani kwao kuendelea kutoa huduma.

Hata hivyo, ratiba hiyo ilivunjwa na msanii wa kike anayefanya vizuri , Vanessa Mdee, ambaye aliwalipia kwenda kulala hoteli ya Hyatt Regency kwa ajili ya kula fungate yao hapo.

Kumleta Uwoya na Dogo hadharani

Wakati wakiwa hawajawahi kuonekana hadharani tangu walipofunga ndoa mwaka jana, wasanii Dogo Janja na Irene Uwoya walionekana kwa mara ya kwanza katika sherehe hiyo.

Dogo Janja na mkewe huyo waliweza kuitwa mbele kwa ajili ya kutoa zawadi, huku Dogo akisema asingeweza kutoa bila ya mkewe kuwepo na kumuita, jambo lililoibua shangwe ukumbini, huku mshereshaji akichombeza kuwa watu bado wanajua ni movie walikuwa wanaigiza.

Japo Uwoya alionekana mwenye aibu kila wakati hata ukaaji wao haukuwa kama mume na mke, lakini Dogo Janja yeye alionekana kujiachia bila wasiwasi na kummwagia Shilole fedha.

Kuwakutanisha harmonise, Sarah na Wolper

Ikiwa imepita muda tangu wasanii Jackline Wolper na Harmonize waachane, harusi ya Shilole iliwakutanisha wawili hao.

Kwani wakati Harmonise akihamishia penzi lake kwa mzungu anayejulikana kwa jina la Sarah, Wolper yeye hivi karibuni amedai kuwa amevalishwa pete ya uchumba.

Hata hivyo, harusi hiyo iliwakutanisha kwa pamoja watatu hao kwa pamoja.

MC awa gumzo

Wakati tumezoea washereheshaji wengi wakiwa wameulambia suti au kuwa nadhifu, kwa Shilole mshehereshaji wake msanii Baba Levo alikuwa tofauti kwani alitupia fulana na suruali ya jeans.

Ukumbi

Kama tulivyozoea masupastaa wengi hufanya harusi kwenye kumbi kubwa na za gharama, lakini kwa Shilole ilikuwa tofauti, kwani alifanya katika uwanja nje na hakukuwa na upangaji mzuri wa viti zaidi watu walikaa kwenye sofa za kiasili.