Manji afunguka mahakamani kuhusu kuvuliwa udiwani

Muktasari:

  • Manji alivuliwa udiwani wa Mdagala Kuu kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu Yusuph Manji anayekabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi amedai mahakamani kuwa hatambui kuvuliwa Udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu kwa sababu hajapewa taarifa wala barua kutoka Manispaa ya Temeke, inayoonyesha kuwa amevuliwa nafasi hiyo.

Manji amesema hayo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati shauri lake lilipofikikwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutanjwa.

"Nimeona taarifa kutoka katika gazeti la Mwananchi kwamba nimevuliwa udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu, kama hii taarifa ni ya kweli... mimi siitambui kwa sababu  nina miezi miwili nipo gerezani na kama wamenivua walipaswa kunipa taarifa,"  alidai Manji.

Manji ambaye alitinga mahakamani akiwa amevalia shati jeupe na suruali ya jinsi nyeusi tofauti na siku nyingine, alidai kwa mwaka mmoja uliopita alitoa Sh 70milioni kutoka  mfuko wake na sio fedha za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi wake, lakini anashangazwa na kitendo cha kuvuliwa udiwani bila kupewa taarifa kwa sababu alichaguliwa na wananchi.

"Mheshimiwa hakimu kesi niliyonayo ni nzito na DPP hapaswi kuangalia upande wake wa kesi tu, kwani anapaswa kuangalia na upande wangu kwa sababu mimi nimechaguliwa na wananchi," alisema.

"Mheshimiwa hakimu, vikao vya awali vya udiwani wa Halmashauri ya  Temeke nilikuwa naudhuria kwa kuwa naheshimu mahakama na kwa uzito wa hii kesi sikutaka kupeleka hata maombi ya dhamana mahakamani," alisema Manji.

Manji alisema anaiomba mahakama imwagize DPP aiambie Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuwa amekamatwa na ndio sababu ya yeye kushindwa kuhudhuria vikao vya madiwani  wa halmashauri hiyo.

Alisema kama hilo haliwezekani, basi wamuandike barua itakayoonyesha agenda ya vikao vyote na yeye atazijibu kwa njia ya barua akiwa gerezani.

"Ninachotambua mimi bado ni Diwani wa Mbagala Kuu na kama nimevuliwa au sijavuliwa udiwani sitambui," alidai

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema kuwa mahakama imepokea hiyo taarifa ya Manji na itaifanyia kazi.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo  hadi Septemba 18, mwaka huu itakapoendelea.

Manji na  wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya Sh 200 milioni na mihuri.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Deogratius Kisinda(28), Abdallah Sangey(46) na Thobias Fwere (43).