Manji atemwa udiwani CCM

Yussuf Manji

Muktasari:

  • Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo alisema jana kuwa kwa mujibu wa sheria, endapo mjumbe bila sababu za kuridhisha au kibali cha maandishi cha mwenyekiti, atakosa kuhudhuria mikutano mitatu ya kawaida ya halmashauri inayofuatana au kamati ambayo yeye ni mjumbe, nafasi yake itakuwa wazi.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Yussuf Manji amepoteza sifa ya kuwa Diwani wa Mbagala Kuu kutokana na kutohudhuria vikao zaidi ya sita vya baraza la madiwani na mikutano zaidi ya mitatu ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke bila ya kutoa taarifa.

Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo alisema jana kuwa kwa mujibu wa sheria, endapo mjumbe bila sababu za kuridhisha au kibali cha maandishi cha mwenyekiti, atakosa kuhudhuria mikutano mitatu ya kawaida ya halmashauri inayofuatana au kamati ambayo yeye ni mjumbe, nafasi yake itakuwa wazi.

“Nawasilisha taarifa rasmi kuwa Manji amekosa sifa ya kuendelea kuwa Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu iliyopo Manispaa ya Temeke, Jimbo la Mbagala na kwamba kata hii itangazwe kuwa wazi.

“Hata vikao na mikutano alivyotoa taarifa alishindwa kuthibitisha taarifa za ugonjwa, kutokana na hilo Manji alivunja kanuni za halmashauri na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura ya 8 ya mwaka 1982 kifungu 25(5) (a) (b) kinaeleza kuwa mjumbe wa baraza la madiwani ambaye hakuudhuria vikao vitatu mfululizo bila ya taarifa ya maandishi kwa mwenyekiti atakuwa amejiondoa katika nafasi ya udiwani,” alisema Chaurembo.

“Napenda nikurejeshe kwenye kanuni za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke za mwaka 2015, Kifungu cha 72 ambacho kinamtaka diwani pamoja na majukumu mengine aliyonayo lazima ahudhurie mikutano ya halmashauri na kamati ndogo ambayo yeye ni mjumbe bila kukosa.”

Chaurembo alisema Manji hakuhudhuria vikao vya baraza la madiwani Februari 3, Machi 24, Juni Mosi, Agosti 25, Novemba 24 vyote vya mwaka 2016 na Februari 14 hadi 15 mwaka huu.

Alisema vikao vingine alivyokosa ni vya kamati ya maendeleo ya halmashauri hiyo ambavyo alikuwa mjumbe vilivyofanyika Machi 18, Agosti 17, Novemba 8 vya mwaka jana na Februari 2 mwaka huu.

Alisema Februari 20, Manji aliandika barua kwa mkurugenzi akitoa taarifa ya kutoweza kuhudhuria vikao vya halmashauri hiyo kutokana na sababu za kiafya bila ya kuwasilisha uthibitisho wa daktari na alikosa vikao baada ya kuandika barua yake vya Machi 3 hadi 4, Mei 18 hadi 19 na Agosti 24 hadi 25.

Machi 2, mkurugenzi wa manispaa hiyo alimwandikia barua akimtaka awasilishe taarifa za daktari kuthibitisha matatizo ya kiafya kama alivyoeleza kwenye barua yake lakini badala yake alikuwa akionekana kwenye vyombo vya habari akiendelea na shughuli zake.

Alisema Mei 25 ndipo Manji alipomwandika barua meya wa halmashauri hiyo na kumpatia nakala yake mkurugenzi akieleza kwamba ameshindwa kuhudhuria vikao vya halmashauri kwa sababu za kiafya bila kuweka uthibitisho wowote.

Chaurembo alisema pia Manji aliweka wazi nia yake ya kutaka kujiuzulu kama hali yake ya kiafya haitaimarika.

Chaurembo alisema ameshamwandikia barua Waziri wa Tamisemi,Geogre Simbachawene kuhusu suala hilo yeye ambaye ndiye mwenye dhamana ya kuweza kupanga uchaguzi mwingine na aitangaze kuwa kata hiyo ipo wazi.