Mapya binti anayesomeshwa urubani na mama kwa kuuza mkaa

Nyamizi Ismail


Muktasari:

Nyamizi Ismail (20), binti anayesomeshwa urubani na mama yake, Bahati Masebu kwa kuuza mkaa, ameendelea kuzungumzia ndoto za maisha yake.

Dar es Salaam. Nyamizi Ismail (20), binti anayesomeshwa urubani na mama yake, Bahati Masebu kwa kuuza mkaa, ameendelea kuzungumzia ndoto za maisha yake.

Jumapili iliyopita katika gazeti hili, Nyamizi alieleza namna urubani ulivyo ndoto ya maisha yake tangu wakati wa uhai wa baba yake aliyefariki dunia mwaka 2013.

Katika mahojiano na Mwananchi, Nyamizi anayesoma katika Chuo cha Tanzania Aviation University (Tauc) kilichopo Tabata jijini Dar es Salaam anasema angependa kusoma chuo maarufu cha urubani barani Afrika. “Mungu akiniwezesha nikapata mfadhili au wafadhili wa kunisaidia kusoma, napenda kwenda kusoma chuo cha 72 Flying School kilichopo Afrika Kusini.”

Novemba 4, Mwananchi kwa mara ya kwanza lilichapisha habari ya mjane, Bahati (41) anayemsomesha Nyamizi urubani ambapo ada yake siyo chini ya Sh100 milioni kwa kazi ya kuuza mkaa. Taarifa hiyo iligusa hisia za wengi na kusababisha vyombo mbalimbali vya habari kumtafuta mama huyo na binti yake kwa ajili ya mahojiano zaidi.

“Kiukweli baada ya kuona taarifa yangu kwenye gazeti la Mwananchi, nilimshukuru Mungu kwanza, sababu sikuamini kama ingeweza kuwa habari kubwa yenye kugusa hisia ya jamii na watu kushangaa kwa nini nimeweza kuthubutu,” anasema binti anayekusudia kutimiza ndoto ya kuwa mmoja wa marubani mahiri wa kike nchini.

“Kwa kweli ninashukuru kwa namna mnavyosaidia jamii, Mungu awabariki daima.”

Nyamizi ni nani?

Akizungumzia tabia yake, binti huyo mwenye haiba ya upole na unyeyekevu anasema nguvu pekee aliyo nayo ni kutokata tamaa.

“Mimi ni mtu wa kawaida ambaye sipendi dharau na kukatishwa tamaa kwa kile nilichodhamiria kukifanya, na ninachukia kuona mtu anapojaribu kuanzisha jambo lake kwa nia njema, wanaibuka watu wanamkatisha tamaa,” anasema.

Anasema Mungu akimjalia anapenda kuwa na mume na watoto watatu.

“Kwenye maisha yangu napenda kuwa mtu mwenye furaha, nionapo kila jambo ninalopitia ninalifaulu kwa uwepo wa Mungu.”

Kiongozi wa kike ampendaye

Kuhusu kiongozi wa kike nchini ampendaye, anasema: “Ni Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, alionyesha uthubutu na amefanikisha na sasa anatuonyesha wazi kwamba mwanamke anaweza, hivyo na mimi nimedhamiria nitaweza kuwa rubani.”

Akizungumzia matokeo baada ya habari yake kutoka gazetini, mama yake Nyamizi, Bahati analishukuru gazeti hili kwa kuandika taarifa zake.

Anasema tangu zilipotoka amekuwa akipigiwa simu nyingi za pongezi kwa namna alivyosimama kwa ajili ya kutimiza ndoto za mwanaye.

“Naomba nikushukuru sana dada (mwandishi) kwa kutangaza taarifa zetu, nilijikuta machozi yananitoka baada ya kusoma ile taarifa na kujiona kumbe mimi ni shujaa,” alisema Bahati.

Kwa yeyote atakayeguswa kumsaidia mama huyo awasiliane naye kwa namba 0674-748841