Marafiki wasimulia kutoweka kwa mwanafunzi wa UDSM

Muktasari:

  • Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitoweka kipindi ambacho kumekuwa na wimbi la utekaji linalofanywa na watu wasiojulikana na baadhi yao hadi sasa hawajulikani walipo.

Dar es Salaam. Marafiki wawili wa mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu juzi usiku wameeleza yaliyojiri kabla ya kutoweka kwake.

Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitoweka kipindi ambacho kumekuwa na wimbi la utekaji linalofanywa na watu wasiojulikana na baadhi yao hadi sasa hawajulikani walipo.

Akizungumza na mwandishi wetu jana , Emmanuel Bernard alisema juzi saa 12 jioni alikuwa na Nondo (26) chumbani kwake katika hosteli za UDSM (Hall 1).

Alisema Nondo alifika chumbani kwake akimweleza kuwa alitoka kwenye mkutano na waandishi wa habari na baada ya muda alisema anakwenda kwao Madale.

“Wakati tukijiandaa kuondoka alipigiwa simu ambayo sikujua ni ya nani. Huku akiendelea kuzungumza aliondoka kwa haraka sikujua alikoelekea,” alisema.

Rafiki mwingine, Malissa Martine alisema Nondo alikuwa akimweleza habari za kutishiwa na watu asiowajua, “Nilikuwa naye kwenye group la Whatsapp linaitwa Maktaba Yetu lakini jana (juzi) saa sita usiku alijitoa.”

Akizungumzia tukio hilo, Mussa Mitumba ambaye ni baba mdogo wa Nondo alisema wanasikitishwa na kitendo cha kijana wao kupotea na kuiomba Serikali kuharakisha uchunguzi ili apatikane.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Jeremiah Jilili akizungumzia tukio hilo alisema wamepokea taarifa za kupotea kwa Nondo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Sayansi ya Siasa (PSPA) na wameripoti ngazi ya utawala.

Jilili alisema Nondo alikabidhi chumba chake Jumatatu kwa uongozi wa chuo baada ya kufungwa wiki iliyopita lakini aliendelea kuonekana chuoni hadi juzi alipotoweka.

“Alikuwa anaonekana hapa na jana (juzi) alikuwepo lakini alikuwa amerudisha chumba kwa waden (msimamizi wa bweni) ukizingatia chuo kimefungwa. Uvumi ulianza kusambaa jana usiku baada ya yeye (Nondo) kuleft kwenye magroup na baadaye akawa hapatikani. Tulichofanya ni kutoa taarifa kwa utawala,” alisema. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema, “Wanafunzi wamefunga chuo, naona kila mmoja ananipigia simu ananiuliza kuhusu suala hilo, msing’ang’anie vitu ambavyo hamna uhakika navyo, kama kuna jambo la muhimu tutalifuatilia, kuweni wavumilivu.”

Mtandao wa TSNP katika mkutano na waandishi wa habari jana ulilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha Nondo anapatikana na pia kufanyia kazi taarifa ambazo amekuwa akizitoa kuhusu watu waliokuwa wanamfuatilia.

Ofisa habari wa mtandao huo, Hellen Sisya alisema kwa mara mwisho Nondo alizungumza na waandishi wa habari juzi akitoa ufafanuzi kuhusu tamko lililotolewa na shirikisho la vyuo vikuu Tanzania (Tahliso) kuhusu kuwapo vikundi vinavyowasemea wanafunzi wa vyuo vikuu.Alisema baada ya mkutano huo, Nondo aliaga kuwa anarejea nyumbani kwao Madale lakini kati ya saa sita na saa nane usiku alijitoa kwenye makundi yote ya WhatsApp.

“Kitendo cha yeye kujitoa kwenye makundi kilitushangaza viongozi wenzake ikabidi tuanze kumtafuta kujua ni nini kimemtokea, mkurugenzi wetu wa sheria alimpigia simu iliita bila kupokewa. Ilipofika saa 9:09 usiku Nondo alimtumia ujumbe mkurugenzi wa sheria akimwambia kuwa yupo hatarini,” alisema.

Hellen alisema baada ya kupata ujumbe waliendelea kumpigia simu na alipopokea hakuzungumza chochote hadi simu ilipokatika na haikupatikana tena.

Alisema viongozi walimtafuta kwa ndugu zake wa karibu waishio Madale na wazazi wake waliopo Kigoma ambao walieleza kutomuona wala kujua taarifa zake.

“Tumetoa taarifa kwa uongozi wa chuo kupitia ofisi ya mshauri wa wanafunzi na polisi tumekwenda ambako walitupatia RB lakini hadi sasa hakuna anayejua mahali alipo mwenyekiti wetu. “Nondo aliwahi kukamatwa na watu waliojitambulisha kwake kuwa ni askari kwa kile walichodai analeta uchochezi na kuhamasisha baadhi ya wanafunzi waliokosa mikopo kuandamana, walimhoji lakini baadaye wakamuachia,” alisema.

Katibu mkuu mstaafu wa mtandao huo, Alphonce Lusako alisema historia ya kutekwa kwa viongozi wa mtandao huo imekuwapo akidai kuwa naye alinusurika kukumbana na hali hiyo mwaka 2017.

Lusako ambaye ni mwangalizi wa haki za binadamu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) alisema inashangaza kuendelea kuwapo kwa genge linaloendeleza vitendo vya utekaji na mauaji ya watu.

Mtandao huo ulipanga kufanya maandamano ya amani Machi 3 kupinga kuuawa kwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini akiwa ndani ya daladala wakati polisi wakitawanya maandamano ya wafuasi wa Chadema eneo la Kinondoni Mkwajuni Februari 16.

Imeandikwa na Cledo Michael, Elizabeth Edward, Fortune Francis na Herieth Makwetta