Matumizi mabaya ya dawa za UTI husababisha uziwi kwa watoto

Watoto waliowekewa vifaa vya kuwasaidia katika usikivu, wakicheza wakati wa mkutano na waandishi wa habari na daktari bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Edwin Liyomba, Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • 1: Mgonjwa aliyepelekwa India mwaka 2003 kwa ajili ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu.
  • 18 : Wagonjwa waliopelekwa India kwa upandikizaji mwaka 2016.

Dar es Salaam. Wataalamu wameonya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya dawa aina ya Gentamyn  inayotibu uambukizo katika mirija ya mkojo (UTI), kwa mama wajawazito husababisha tatizo la uziwi kwa watoto wanaozaliwa.

Takwimu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zinaeleza kuwa zaidi ya asilimia 95 ya wagonjwa walioathiriwa na tatizo hilo la uziwi ni watoto wadogo ambao walizaliwa wakiwa hivyo.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo (ENT) kutoka MNH, Edwin Liyombo alisema madhara ya uziwi kwa watoto hutokana na dawa mbalimbali wanazotumia wajawazito ambazo hugeuka sumu kwa masikio ya watoto.

Alisema dawa hiyo ya gentamyn, iwapo mama anayeumwa UTI ataitumia pasipo kufuata kanuni alizopewa na daktari, hugeuka sumu na kuathiri mfumo wa masikio ya mtoto aliye tumboni.

“Wanawake wanapokuwa wajawazito mara nyingi husumbuliwa na tatizo la maambukizi katika njia ya mkojo na wengine malaria hivyo mama akitumia dawa aina ya Quinnine (kutibu malaria) hizi mara nyingi zina sumu, mama akinywa vibaya anaweza kupata tatizo,” alisema.

Dk Liyombo alisema ikiwa mama hatakuwa mwangalifu wakati mtoto anazaliwa na akapata maambukizi katika kitovu, asipotibiwa vizuri pia anaweza kupata tatizo la uziwi iwapo hatatibuwa kwa usahihi.

“Ugonjwa wa manjano pia huleta sumu ambayo inaweza kusababisha madhara kwenye masikio,” alisema.

Kutokana na hatari hiyo, mmoja wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji, Bupe Mwakalindile alishauri wazazi kuwa makini na watoto kwani kuna umri ukifika mtoto lazima awe amejua mambo kadhaa ikiwamo kujifunza kuzungumza, hivyo wakiona hana dalili wamfikishe kwa wataalamu haraka ili afanyiwe vipimo na kuwekewa kifaa cha kumsaidia.

“Nilipopata taarifa za mtoto wangu kuwa na ulemavu wa kusikia nilijisikia vibaya, ukiangalia safari ya mimba miezi tisa mpaka kujifungua halafu unakutana na wataalamu wanakwambia mtoto kiziwi, tunashukuru alipata tiba na yupo vizuri sasa anasoma chekechea ila kuna changamoto nyingi kwa kweli,” alisema Bupe.

Upandikizaji vifaa vya kusikia kuanza Juni

Kuhusu tiba ya upasuaji, Dk Liyombo alisema MNH itaanza rasmi kutoa huduma hiyo kwa watoto wasiosikia na kuwawekea vifaa vya usikivu (Cochlea Implant), mwezi ujao.

Alisema asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo, hivyo wanatarajia huduma hiyo kusaidia watoto wengi nchini na pia kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani ya nchi. 

“Gharama imekuwa ni kubwa kwa mzazi kutoka hapa kwenda India tukafikiria nini tunaweza kufanya ili kusaidia, tulishaanza kufanya mipango ya kusogeza huduma kwa kuanza na matengenezo ya vifaa walivyowekewa ‘mapping’ tunaendelea na sasa tunakuja na upasuaji kufikia Juni,” alisema.

Dk Liyombo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Masikio, Pua na Koo (ENT) alisema gharama za kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja ni kati ya Sh80 hadi 100 milioni anapopelekwa nje ya nchi.