Matumizi ya intaneti yachangia kukua sekta ya utalii

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa kuongezeka kwa watumiaji wa mtandao wa intaneti kumechochea kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya utalii nchini.

Hayo yameainishwa kwenye ripoti mpya ya utalii Tanzania ya mwaka 2016 iliyotolewa jana na Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, inayojihusisha na huduma za hoteli na usafiri kwa watalii.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Meneja Mkazi wa kampuni hiyo nchini, Fatema Dharsee alisema idadi kubwa ya Watanzania kwa sasa wanatumia intaneti kwenye simu za mkononi na kompyuta kutafuta huduma za hoteli jambo linaloleta ishara nzuri kwa sekta ya utalii.

“Tanzania mpaka hivi sasa ina watumiaji wa intaneti zaidi ya milioni 19 kufikia mwaka 2016 kutoka milioni 17 mwaka 2015. Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.9 kwa mwaka na ueneaji wa mtandao wa intaneti wa asilimia 83 miongoni mwa Watanzania milioni 50 nchi nzima,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Utalii Tanzania, Denis Simkoko alisema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za wadau mbalimbali kuhakikisha sekta ya utalii inafanikiwa na kuleta matokeo chanya.

“Bila shaka mafanikio tuliyonayo kwa sasa katika sekta ya utalii nchini ni matokeo mazuri ya ushirikiano wa karibu baina ya Serikali na wadau wengine.

“Shirikisho la Utalii Tanzania lipo kama daraja katika kuwaunganisha wadau mbalimbali wa sekta hii nchini kote na wizara husika yenye mamlaka kwa mujibu wa Serikali,” alisema.