Mauzo, uzalishaji Tanzanite kuongezeka

Muktasari:

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Zena Kongoi alisema jana kuwa wanatarajia mnada wa madini hayo kufanyika kila baada ya miezi mitatu ili kuongeza tija ya soko lake.

Mirerani. Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limejipanga kuhakikisha uzalishaji na mauzo ya madini ya Tanzanite yanaongezeka ili kulipa kodi na kuipatia mapato mengi Serikali.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Zena Kongoi alisema jana kuwa wanatarajia mnada wa madini hayo kufanyika kila baada ya miezi mitatu ili kuongeza tija ya soko lake.

Kongoi alisema hayo wakati wajumbe wapya wa bodi ya Stamico walipotembelea mgodi wanaoumiliki kwa pamoja na Kampuni ya TanzaniteOne uliopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.

“Serikali kupitia Stamico tunamiliki mgodi huo kwa asilimia 50 na TanzaniOne asilimia 50, hivyo tunataka kupiga hatua zaidi ili kuhakikisha Taifa linafaidika na wananchi wanafaidika,” alisema Kongoi.