Mbowe amshangaa Waziri Ummy Mwalimu

Muktasari:

 

  • Ameelezea kilichotokea hadi wakampeleka Lissu Nairobi kwa gharama zao

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemshangaa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kusema kuwa Serikali iko tayari kumtibu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu popote duniani.

Mbowe ametoa mshangao huo leo Ijumaa alipokuwa akitoa taarifa kuhusu matibabu ya Lissu yanayoendelea jijini Nairobi.

Amesema wakati walipoamua kumpeleka Lissu jijini Nairobi, Waziri Ummy alikuwepo lakini walitaka Lissu apelekwe Muhimbili.

Mbowe amesema wanachama, watu mbalimbali wamechangia matibabu ya Lissu ikiwa ni hata wanachama wa vyama vingine walioguswa na tukio hilo.

“Sasa wiki mbili baadaye ndio anatoka Waziri wa Afya anasema Serikali iko tayari kumtibu popote duniani, eh kweli? Mama Ummy Mwalimu anasahau kauli yao wakinieleza mimi pale Dodoma, wamuogope Mungu, walikataa ‘categorically’  pengine walifikiri wao ni miujiza mheshimiwa Lissu kupona na sisi tulisema lazima tumpeleke Nairobi ndiyo mahali tunaona kweli kunawezekana kukaokoa yale maisha,”amesema Mbowe.

“Ilikuwa ni hatari na ni maamuzi yalikuwa magumu sana, watu ambao wana mamlaka, Waziri wa Afya yuko pale, Spika yuko pale nawaambia fanyeni maamuzi tumuokoe huyu mtu wanasema hatuwezi kumpeleka Nairobi, mimi nikasisitiza sisi tunampeleka Nairobi wakasema basi utalipa mwenyewe, nikasema sawa tutalipa wenyewe.”

Mbowe amesema hiyo ni hali halisi ambayo ameona awaambie Watanzania.