Mbowe ataka uchunguzi wa aliko Azory Gwanda

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameitaka Serikali kutoa tamko kuhusu aliko mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Azory Gwanda.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mbowe alisema kitendo cha Serikali kukaa kimya kinaleta wasiwasi kwa ndugu na jamii ya wanahabari.

“Sasa ni wiki ya tatu tangu Azory ametoweka nyumbani kwake, lakini Serikali haijatoa tamko lolote, hatuelewi nini kimemtokea,” alisema.

Azory (42), anayefanya kazi za uandishi wa habari Kibiti na Rufiji mkoani Pwani ametimiza siku 22 tangu atoweke kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana Novemba 21.

Mbowe alisema kumekuwa na matukio ya kutisha kama watu kupotea na maiti kuokotwa zikiwa zimefungwa kwenye mifuko hali ambayo inawatia wasiwasi wananchi.

“Tunaomba vyombo vya dola kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika ili kufahamu aliko mwandishi huyo,” alisema.

Mbali ya wito huo, mwenyekiti wa Baraza Kuu la CUF, Julius Mtatiro alisema kufungia vyombo vya habari kwa sababu vimekosea kuandika takwimu si halali.

Alisema makosa ya takwimu yanatakiwa kusahihishwa lakini si kukifungia chombo cha habari kwa kuwa madhara yake ni watu kukosa ajira hata ambao hawakuhusika moja kwa moja na makosa yaliyofanywa.