Mbunge: Mauaji Pwani yamepangwa

Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (kushoto) na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega wakiagana na wenzao katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • “Nataka niseme na Rais wangu ajue. Mambo haya yanayotokea, hayatokei kwa bahati mbaya. Mambo haya yana root cause (kiini chake). Mambo haya yamepangwa,” alisema mbunge huyo na kuongeza:
  • “Yapo mambo mengi, zipo chuki nyingi zimejengwa kwa wananchi. Yapo mambo mengi yalifanyika yanatoa kero kubwa kwa wananchi ndio maana gazeti la leo (Mwananchi) lilipoandika taarifa hizi, mimi sikushangaa kwa sababu ninajua yako hayo mambo.”

Dodoma. Mauaji katika wilaya za Kibiti na Rufiji jana yaliibuka bungeni kwa mara ya pili, wakati mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa alipoeleza siri ya mipango na kiini chake.

“Nataka niseme na Rais wangu ajue. Mambo haya yanayotokea, hayatokei kwa bahati mbaya. Mambo haya yana root cause (kiini chake). Mambo haya yamepangwa,” alisema mbunge huyo na kuongeza:

“Yapo mambo mengi, zipo chuki nyingi zimejengwa kwa wananchi. Yapo mambo mengi yalifanyika yanatoa kero kubwa kwa wananchi ndio maana gazeti la leo (Mwananchi) lilipoandika taarifa hizi, mimi sikushangaa kwa sababu ninajua yako hayo mambo.”

Mbunge huyo alisema yako mambo Serikali inapaswa kuyafanya na iwe sasa kwa sababu jambo hilo ni kubwa, linaendelea kutanuka kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

  Mchengerwa alitoa kauli hiyo jana baada ya Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini kuomba mwongozo kwa kutumia kanuni ya 47(1), akitaka Bunge liachane na shughuli za mezani na kujadili usalama katika maeneo hayo.

Mbunge huyo alisema Waziri Mwigulu alipotembelea maeneo hayo alitoa maagizo mazuri, lakini yametafsiriwa vibaya na polisi ambao wanakamata na kupiga watu hovyo.

“Hivi karibuni walimkamata Sultani Mpiji aliyekuwa akifua nguo. Baba yake amekuta maiti yake Muhimbili. Wananchi wanalalamika, wananchi wanahamahama, hali si nzuri. Hali ni mbaya sana,” alisema.