Mdee asema wanawake ni chachu ya ushindi Uchaguzi Mkuu 2020

Muktasari:

  • Mbunge Mdee amesema wanawake wamekuwa wakitumika kama daraja pasipo wao kujijua.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee amesema wanawake wakiwezeshwa na kupewa mafunzo ya kujitambua watakuwa chachu ya ushindi mwaka 2020.

Akizungumza na wanawake wa jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam leo Jumapili Oktoba 22,2017 amesema wamekuwa wakitumika kama daraja pasipo wao kujijua.

Mdee amesema kutokana na idadi kubwa ya wanawake waliopo kuliko wanaume, wakiamua kufanya mageuzi wanaweza ila inahitajika kwanza kujengewa ujasiri.

"Wanawake wakijitambua na hasa kwa kupatiwa mafunzo na ujasiri wataweza kuwa mkombozi katika Uchaguzi Mkuu 2020," amesema.

Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe amesema kupitia semina hiyo wanawake hao watajua nafasi zao katika jamii na kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi wowote wenye tija.

"Unapoona matukio ya ajabu yanatokea, watu wanapotea, Kamanda wetu Lissu (Tundu Lissu) anapigwa risasi na anapona ujue Mungu ana makusudi naye, hivyo nasi wanawake tujue cha kufanya," amesema. Mwenyekiti wa Bawacha wa jimbo hilo, Agnester Lambati amesema, ''Tumeamua kumwita Mdee aje kuzungumza na wanawake wa Segerea tukitambua mchango wake wa kuwapigania wanawake wa nchi hii."

Awali, Mdee alifungua ofisi ya Bawacha ya jimbo hilo na kumkabidhi kadi ya uanachama Florence, ambaye ni mke wa Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Ilala, Dk Makongoro Mahanga.