Meja Jenerali Milanzi astaafu utumishi wa umma, aiaga wizara

Muktasari:

  • Baada ya miaka mitatu ya kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenrali Gaudence Milanzi amestaafu. Kuanzia Septemba 16, kamand ahuyo amestaafu jeshini na utumishi wa umma kwa ujumla.

Dodoma. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanyakazi kwa weledi ili kuogeza tija kwa Taifa.

Katibu mkuu huyo ametoa rai hiyo leo, Septemba 25, 2018 alipokuwa akiwaaga watumishi wa wizara baada ya kustaafu jeshini na kwa mujibu wa sheria tangu Septemba 16.

Milanzi amesemwa kwa muda wote aliitumikia wizara hiyo alipata ushirikiano wa kutosha uliomuwezesha kuiongoza vyema wizara hiyo na kuchangia mafanikio yaliyojidhihirisha kwenye sekta za wanyamapori, utalii, misitu na nyuki na malikale.

Katika kipindi cha uongozi wake wizarani hapo, amesema wizara imepata mafanikio katika  vita dhidi ya ujangili.

“Tumekamilisha mambo mengi. Kila mmoja wenu alikuwa akinisaidia ili wizara isonge mbele. Hakuna aliyetaka kunikwamisha. Ninawashukuru sana,” amesema Milanzi.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kumuaga Milanzi iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Dodoma, kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Aloyce Nzuki amempongeza kwa utumishi wake.

“Umeweka mifumo mizuri na kubuni mikakati na mbinu za kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili wizara na kuhakikisha watumishi wanapata utulivu wa akili kwa kujali maslahi yao. Uliwawezesha kufanya kazi wakiwa watulivu wa akili jambo liliongeza ufanisi kazini,” ameeleza Dk Nzuki.

Milanzi aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara hiyo Disemba 2015. “Nashukuru nimestaafu salama. Wizara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na inagusa masilahi ya wengi. Jukumu nililopewa lilikuwa kusimamia maslahi ya nchi, naamini kuna masilahi ya watu yalivurugwa hivyo mimi kuwa mwiba kwao,” amesema akiaga kamanda huyo wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).