Meya Tanga akubali yaishe

Muktasari:

Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapha (Selebosi) amesema kuwa mvutano huo umekwisa baada ya halmashauri kuketi na wamiliki hao na kuwapa sharti la kupitia katika kituo kikuu kipya cha mabasi cha Kange.

 Hatimaye halmashauri ya jiji imemaliza mvutano uliodumu kwa muda mrefu kati yake na wamiliki wa mabasi yanayofanya safari kwenda wilaya za Mkinga na Pangani kwa kuruhusu yapitie katika vituo ilivyokuwa imevizuia.

Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustapha (Selebosi) amesema kuwa mvutano huo umekwisa baada ya halmashauri kuketi na wamiliki hao na kuwapa sharti la kupitia katika kituo kikuu kipya cha mabasi cha Kange.

Mustapha amesema halmashauri hiyo ilikuwa imezuia mabasi yaendayo wilaya za Mkinga na Pangani kuegeshwa na kukaa kwa muda mrefu katika vituo vya Mwembe Mawazo, Chumbageni na Mwembeni Mabawa kwa sababu si rasmi.

 

“Baada ya kuhamia Kituo Kikuu cha Kange, wenye mabasi walituletea usumbufu wa kuendelea kutumia kituo cha zamani cha Ngamiani huku mabasi ya Mkinga yakitumia Mwembemawazo na Pangani Mwembeni Mabawa jambo ambalo lilisababisha kero kwa wenye nyumba,” amesema.

Amesema baada ya Mkuu wa Mkoa kuingilia kati sasa halmashauri imeruhusu mabasi yaendayo Wilaya za Mkinga na Pangani kutumia vituo hivyo lakini kwa sharti la kuhakikisha kila basi linapitia Kituo Kikuu cha Kange ili kulipa ushuru.

“Tumeruhusu kwa muda mfupi mabasi hayo kutumia vituo tulivyokuwa tumepiga marufuku kwa sababu tuna mipango ya muda mrefu ya kujenga vituo vya kisasa kwa ajili ya mabasi yanayofanya safari maeneo hayo,” amesema.

Dereva wa basi aina ya Coaster linalofanya safari katika ya Tanga na

Horohoro, Shaaban Ali, amesema, “tunampongeza Meya wa Jiji la Tanga kwa kukubali tutumie vituo vya Mwembe Mawazo na Mwembeni kwa sababu ilikuwa ni usumbufu mno kwa abiria.”