Mgombea asema mahabusu imemuongezea ari ya ushindi

Muktasari:

Amekaa mahabusu kwa siku tano kutokana na kukabiliwa na kesi ya kujeruhi.

Mwanza. Mgombea udiwani Kata ya Mhandu (Chadema), Godfrey Misana amesema siku tano alizokaa gerezani Butimba jijini Mwanza zimemuongezea ari, nia na ujasiri wa kushinda katika uchaguzi mdogo Novemba 26,2017.

Kwa siku tano kuanzia Novemba 17,2017 hadi jana Jumanne Novemba 21,2017 alikuwa mahabusu kutokana na kesi inayomkabili akidaiwa kujeruhi.

Akihutubia mkutano wa kampeni eneo la Machinjioni jijini Mwanza jana muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana katika shauri la jinai namba 540/2017 la kumjeruhi meneja wa kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba, mgombea huyo amesema kunyimwa dhamana na kupelekwa mahabusu hakujamdhoofisha, bali kumemuimarisha.

"Muda wote niliokaa mahabusu nimepata ushirikiano na kutiwa moyo na kila mmoja; nadhani ni mipango ya Mungu mimi kwenda mahabusu ili Chadema inyakue kiti hiki,” amesema.

Amesema kwa kipindi alichokaa gerezani, amepata wafuasi zaidi ya 2,800 miongoni mwao wakiwa mahabusu na wafungwa.

“Chadema inapendwa hadi gerezani na wafungwa na mahabusu ambao kwa siku zote wamenitia moyo wa kutokata tamaa,” amesema Misana.

Meneja kampeni wa mgombea huyo, Charles Chinchibela ambaye pia alikuwa mahabusu amewasihi wakazi wa kata hiyo kuwapa pole kwa madhila yaliyowafika kwa kumpigia kura Misana kuwa diwani wao.

“Tumefunguliwa kesi na kupelekwa mahabusu kwa kutetea haki ya wakazi wa Mhandu ya kupata maji safi na salama, huduma bora ya afya na miundombinu ya barabara; tulipeni kwa kumchangua mgombea wa Chadema,” amesema Chinchibela.

Misana, Chinchibela na watu wengine wawili wameachiwa kwa dhamana baada ya Hakimu Mkazi Ainawe Moshi kutupilia mbali pingamizi la dhamana lililowasilishwa na Wakili wa Serikali, Elizebeth Barabara.

Moshi, ambaye ni hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza alikubali hoja za mawakili wa utetezi Gasper Mwanaliela na Paul Kipeja kuwa shauri linalowakabili wateja wao lina dhamana na hakuna hoja za msingi za kuizuia.