‘Soka la Barca litaiua Yanga Jumamosi’

Muktasari:

  • Ni ubashiri wa kocha wa Stand United, Pluijm, Omog wakomaa

Dar es Salaam. Pamoja na Yanga kujaribu kucheza soka kama la Barcelona ya Hispania, kocha wa Stand United, Patrick Liewig ameipa  nafasi Simba kushinda mchezo huo wa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha huyo wa zamani wa Simba aliyeiongoza timu yake kuifunga Yanga bao 1-0, Jumapili iliyopita alisema aina ya wachezaji wa Simba endapo watacheza kwa utulivu, umakini wanayo nafasi kubwa ya kuifunga Yanga.

“Nimeiongoza timu yangu kucheza na Yanga, nimegundua udhaifu wao, japo kwa kiasi fulani wanajaribu kucheza soka kama la Barcelona, lakini bado hawajafikia huko, ni jambo linalowapa shida,” alisema kocha huyo Mfaransa.

“Nimeiangalia Simba mara moja, inajaribu kucheza soka la kuvutia, inao wachezaji wanaowajibika uwanjani na wanajua nini wanachokifanya bila kujali wameshinda au la.

“Nikijaribu kuangalia aina ya uchezaji wa timu zote mbili kuelekea mechi yao ya Jumamosi, naipa Simba nafasi kubwa ya kushinda, ingawa simaanishi kuwa Yanga si timu bora, lakini kwa uchezaji wa Simba msimu huu, Yanga inapaswa kufanya kazi ya ziada,” alisema Liewig ambaye mkataba wake na Stand umefikia mwisho.

Wakati Mfaransa huyo akibashiri ushindi kwa Simba, kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema jana kuwa hana hofu na Simba licha ya kwamba anawaheshimu kuwa ni timu nzuri, lakini anaamini wakitoka Pemba mambo yatakuwa mazuri kama ilivyokuwa msimu uliopita.

“Tunatakuwa kusahau kuhusu matokeo ya mchezo uliopita na sasa tuangalie mchezo ujao kuhakiksiha tunapata pointi. Naamini kambi ya Pemba itarejesha morali ya wachezaji wangu na kuirejesha timu yangu katika ubora tunapoelekea kuwakabili wapinzani wetu.”

Mpinzani wake, Joseph Omog ameendelea kulia na wachezaji wake kupoteza nafasi na kuahidi kuwa hilo ndilo jambo muhimu atakalolifanya kazi katika kambi iliyoko Morogoro kwani anataka ushindi dhidi ya Yanga.

“Nafurahi kuona tunatengeneza nafasi, lakini tatizo wachezaji wangu hawatumii zote, jambo  hilo linaniumiza kichwa na lazima tulifanyie kazi kabla ya kuivaa Yanga.

Tiketi za kielektroniki kuuzwa leo

Mashabiki wa soka wanaotarajia kutazama mchezo huo wa Ligi Kuu Jumamosi wameshauriwa kuanza kununua tiketi kwa njia ya  kieletroniki kuanzia leo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Jana, kampuni inayosimamia mchakato wa tiketi za hizo,  Selcom ilikutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vyombo vya usalama na wasimamizi wa Uwanja wa Taifa kujadili suala hilo pamoja na uuzaji wa tiketi za mchezo huo.

Akizungumzia suala la tiketi, meneja miradi wa Selcom, Gallus Runyeta alisema mashabiki wote wanaotarajia kushuhudia mchezo huo waanze leo kununua tiketi mapema katika vituo vilivyopo Chang’ombe, vituo vyote vya mafuta vinavyomilikiwa na Kampuni za Puma na Total na mawakala waliopo maeneo mbalimbali ya jiji.

“Tumeainisha maeneo hayo ili mashabiki wanaotarajia kuangalia mchezo  huo wanunue tiketi mapema. Shabiki atakayekuwa na tiketi yake siku ya mchezo atapewa kadi bila kulipia,” alisema Runyeta na kuahidi kuwa kampuni yake  itatumia vyombo vya habari na vipeperushi ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfumo huo.

Awali,  ofisa habari na nawasiliano wa  TFF, Alfred Lucas  mbali na kubainisha kuwa maandalizi ya mchezo wa watani yanaendelea  vizuri, alisema TFF inaunga mkono matumizi ya tiketi za kielektroniki kwa asilimia 100.

“Mfumo huu hauwezi kuzuilika kwa sasa na ndiyo maana TFF inaungana na wote wanaohusika kuhakikisha mfumo huu unafanya kazi kwa mafanikio.”

Mkurugenzi wa michezo, Alex Nkenyenge alisema sasa ni wakati mwafaka kwa viongozi wa klabu, mashabiki na wadau wa soka kudumisha utamaduni wa kulipa viingilio ili kuziwezesha klabu kuvuna mapato ya kutosha.

“Tumewekeza fedha nyingi katika mfumo huo, tunaamini ni wakati mzuri wa kuachana na mambo ya ujanja ujanja. Viongozi wa klabu na mashabiki wawe na utamaduni wa kulipa viingilio,” alisema.

Viingilio

Tiketi za kushuhudia mchezo huo unaovuta hisia za wapenzi wa soka nchini  zimepangwa kuwa ni Sh30,000 kwa VIP A, VIP B na C ni  Sh20,000 na viti vya rangi ya chungwa itakuwa Sh7,000.

Imeandikwa na Imani Makongoro, Oliver Albert na Fredrick Nwaka.