Thursday, April 20, 2017

 

Herrera: Hazard ni habari nyingine
MANCHESTER, ENGLAND
JUMAPILI iliyopita ni kama alimtia mfukoni wakati Manchester United ilipocheza na Chelsea kwenye Ligi Kuu England uwanjani Old Trafford, kiungo staa wa mchezo, Ander Herrera ameibuka na kudai kwamba Eden Hazard ni bonge la mchezaji duniani kwa sasa.

Herrera, alimfunika kabisa Hazard kwenye mechi hiyo, ambapo alikuwa akimkaba hadi kivuli, kwa upande wake anamwona Mbelgiji huyo kuwa ni mchezaji bora kwa mwaka huu. Licha ya kufanya majukumu ya kumdhibiti Hazard, kwenye mechi hiyo, Herrera alipiga asisti ya bao la kwanza kabla ya yeye mwenyewe kupiga la pili wakati Man United ilipoibuka na ushindi wa 2-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Herrera alisema hivi: "Kwa maoni yangu, Eden Hazard ni mchezaji bora kabisa kwenye ligi mwaka huu. Ni mmoja pia wa wachezaji bora duniani. Baada ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, basi wanafuatia Neymar, Eden Hazard, Antoine Griezmann na Paul Pogba."


Herrera akafichua kitu kingine kwamba hawezi kuuzima moto wake alioanzisha kwa sababu hofu yake ni kupoteza namba katika kikosi cha kwanza cha Man United.


"Soka linabadilika. Hapa kuna wachezaji mahiri, lakini Man United bado itasajili wachezaji wengine wakubwa. Hivyo, silali, tizi tu na kucheza kwa sababu, nitafanya kile ambacho kocha anataka kutoka kwangu," alisema.


"Kwangu mimi, timu ndiyo muhimu. Kila mechi ni fainali, hivyo tunapaswa kupigana pamoja. Imani ni kubwa kabisa kwamba tutatinga kwenye Top Four na tutabeba taji la Europa Ligi pia."

-->