Algeria yasubiri muujiza

Muktasari:

Timu hiyo inayoongozwa na mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika, Riyad Mahrez ni lazima wawafunge vinara wa Kundi B, Senegal huku wakiomba vibonde wenzao Zimbabwe waifunge Tunisia mjini Libreville kufufua matumaini yao.

Franceville, Gabon. Algeria iliingia katika fainali za Mataifa Afrika Gabon ikiwa moja ya timu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa, lakini leo inahitaji miujiza mjini Franceville ili kufuzu kwa robo fainali.

Timu hiyo inayoongozwa na mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika, Riyad Mahrez ni lazima wawafunge vinara wa Kundi B, Senegal huku wakiomba vibonde wenzao Zimbabwe waifunge Tunisia mjini Libreville kufufua matumaini yao.

Matokeo hayo yatazifanya Algeria na Zimbabwe kugongana katika nafasi ya pili wakiwa na pointi nne kila moja, hivyo kusubiri tofauti ya mabao kuamua timu itakayosonga mbele.

Kwa kuangalia mechi nne zilizochezwa mjini Franceville hadi sasa ni vigumu kwa Algeria na Zimbabwe kupata ushindi rahisi kutoka kwa Senegal na Tunisia.

Senegal imejihakikisha kumaliza kinara wa kundi na sasa inajiandaa kucheza na mshindi wa pili wa Kundi A mjini Gabonese.

Tunisia inahitaji sare tu dhidi ya Zimbabwe kujihakikisha nafasi ya pili ili acheze na vinara wa Kundi A mjini Libreville.

Kocha wa Algeria, Georges Leekens anajua kuwa kikosi chake kinakabiliwa na ushindani mkali leo.

“Senegal inacheza mpira mzuri unaovutia, ningependa tungekuwa tumefuzu kabla ya kucheza nao,” alikiri kocha Leekens.

Kocha wa Senegal, Aliou Cisse alisema hatowapumzisha nyota wake wa kikosi cha kwanza, kwa lengo la kuhakikisha wanamaliza katika nafasi ya kwanza.

“Tutawatumia wachezaji wetu wote, hii mechi ni muhimu kwetu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Cisse.