Casilas wala hana presha ya usajili

Muktasari:

Casilas aliongeza kukaa kwake nje kwa muda mrefu hakujamfanya abweteke na badala yake alikuwa akijifua na timu yake ya mtaani na muda mwingine katika mazoezi ya gym ili kujiweka fiti asije akaongezeka uzito.

Dar es salaam. Kipa Hussein Sharif ‘Casilas’ amesema hana presha katika kipindi hiki cha usajili, kutokana na kuwa na mipango yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Muda huu ninachofanya katika kipindi hiki nimetuliza tu akili yangu kwa sasa, kwa sababu kuna mipango yangu ya kucheza soka nje ambayo ilikuja baada tu ya kusimamishwa nikiwa Kagera kwahiyo ikikaa sawa naondoka muda wowote,”alisema.

Casilas aliongeza kukaa kwake nje kwa muda mrefu hakujamfanya abweteke na badala yake alikuwa akijifua na timu yake ya mtaani na muda mwingine katika mazoezi ya gym ili kujiweka fiti asije akaongezeka uzito.

“Najitambua kuwa bado nina muda mwingi wa kucheza, na sijakata tamaa na ndio maana hata baada ya kutoka katika ligi kuu nilikuwa najifua na timu ya mtaani huku Kinondoni, pia nilikuwa naingia gym kikubwa ni kulinda kiwango changu na kuongezeke uzito usiokuwa na faida,”alisema.

Akizungumzia kuhusu timu za Ligi Kuu ambazo zinahitaji saini yake, licha ya kuwa ana dili la kutoka nje ya nchi alisema kuwa kuna klabu tatu ambazo zimeonyesha nia ya kumuhitaji, lakini bado hajakuwa na jibu kamili wapi anaweza kutua.

“Nashindwa kufanya uamuzi hivi sasa kwa sababu ya dili langu la nje, na dili hili lilianza muda mrefu kabla hata ya hivi klabu tatu za bongo kuja, hivyo naangalia kama nje ikishindikana basi naweza nikasaini katika moja ya hivi vilabu,” alisema kipa huyo wa zamani wa Mtibwa, Simba na Kagera Sugar.

Hata hivyo inatajwa kuwa kipa huyo kama ikishindika kwenda nje ya nchi anaweza akarejea katika kikosi chake cha zamani cha Mtibwa baada ya aliyekuwa kipa wa timu hiyo Said Mohammed ‘Nduda’ kusajiliwa na Simba.