Fifa yaanika adhabu zinazoikabili Yanga

Muktasari:

  • Miongoni mwake ni faini ya Sh31 milioni, endapo Fifa haitokubaliana na utetezi wa Yanga wa kutokamilisha usajili huo ndani ya muda uliopangwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa uhamisho wa wachezaji kwa ligi ya ndani (DTMS).

Dar es Salaam. Suala la Yanga kuchelewesha usajili wa ndani hadi baada ya Agosti 6 limechukua sura mpya baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kubainisha adhabu tatu tofauti zinazoikabili klabu hiyo.

Miongoni mwake ni faini ya Sh31 milioni, endapo Fifa haitokubaliana na utetezi wa Yanga wa kutokamilisha usajili huo ndani ya muda uliopangwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa uhamisho wa wachezaji kwa ligi ya ndani (DTMS).

Timu hiyo na Coastal Union iliyoko Ligi Daraja la Kwanza ndizo pekee nchini zilizoshindwa kukamilisha usajili wao Agosti 6, siku ya mwisho kwa dirisha la usajili kwa wachezaji wa ndani kufanyika.

Barua iliyoandikwa Machi 6, 2015 na aliyekuwa katibu mkuu wa Fifa, Jerome Valcke  kwenda kwa wanachama, shirikisho hilo limetaja adhabu za aina tatu tofauti zinazotolewa kwa makosa yanayohusiana na usajili kwa mfumo huo.

Adhabu hizo ni kuonywa, karipio kali pamoja na kutozwa faini ya Faranga 14,000 za Uswisi, ambazo ni sawa na Sh31 milioni za Tanzania.

Awali, kulienea taarifa kuwa Yanga na Coastal zinaweza kushushwa daraja kutokana na kufanya kosa hilo. Hata hivyo, maelekezo hayo ya Fifa yanaendana na kauli ya Katibu Mkuu wa  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa aliyesema juzi Yanga inaweza kutozwa faini kutokana na kosa hilo.

“Baadhi ya klabu zetu zimewahi kupata moja kwa moja adhabu kutoka Fifa kutokana na kutofanya usajili vizuri na ninakumbuka Yanga iliwahi kuadhibiwa kwa usajili wa Mbuyu Twite.

“Hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kupigwa faini kutokana na kuchelewa huko,” alisema Mwesigwa ambaye pia alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha Yanga kuwa TFF siyo wahusika wakuu wa mfumo huo wa usajili, bali wao ni kama kiunganishi kati ya klabu na Fifa.

“Hili dirisha siyo TFF inayoamua, inaweza kuomba kwa Fifa, lakini wanaoweza kuamua ni Fifa na siyo TFF,” alisema Mwesigwa juzi alipozungumza na gazeti hili.  

Awali, shirikisho hilo la kimataifa lilipongeza Shirikisho la Soka Nigeria (NFF) pekee Afrika kwa kukamilisha kwa wakati usajili wa klabu zake zote kwa ajili ya ligi ya nchi  hiyo.

Taarifa ya Fifa ilitoa pongezi na kutangaza kuwa Nigeria ni nchi ya kwanza Afrika kutumia mfumo wa DTMS tangu ulipoasisiwa mwaka 2010 katika mkutano mkuu wa Fifa, lakini ukaanza ule wa wachezaji kuhama kutoka shirikisho moja kwenda jingine (TMS) unaoendelea hadi Septemba 6.

Umuhimu wa matumizi ya DTMS ni kwa shirikisho (TFF) kufuatilia kila uhamisho wa mchezaji na kutatua matatizo ya usajili kirahisi kama kutatokea matatizo.

Hata hivyo, kauli ya Fifa ya Julai 5 katika pongezi za NFF, ilisema katika taarifa yake kuwa mashirisho mengine wanachama kupitia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wanatarajiwa kuanza kutumia njia hiyo kwa ajili ya usimamizi wa wachezaji wa ligi zao za ndani