Januari ni njema kwa ‘SamaGoal’

Nyota ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea RCK Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ‘SamaGoal’ inaonekana kung’ara zaidi mwezi huu wa Januari kulinganisha na miezi mingine.

Muktasari:

  • Ndani ya miaka miwili sasa, Samatta amekuwa akipata mafanikio zaidi mwezi huo, kabla na hata baada ya kujiunga na Genk.

Dar es Salaam. Nyota ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea RCK Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ‘SamaGoal’ inaonekana kung’ara zaidi mwezi huu wa Januari kulinganisha na miezi mingine.

Ndani ya miaka miwili sasa, Samatta amekuwa akipata mafanikio zaidi mwezi huo, kabla na hata baada ya kujiunga na Genk.

Mapema mwaka jana, Samatta alitangazwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwa mwaka 2015, ambayo aliipata mwezi huo.

Mwezi huo huo Januari mwaka jana, Samatta alijiunga na KRC Genk kutoka TP Mazembe, na kuweka rekodi ya Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu Ubelgiji.

Kama ilivyokuwa mwaka jana, nyota hiyo imeendelea kumuwakia Samatta mwaka huu, ambapo amefanikiwa kwa mara ya kwanza kucheza kwa dakika nyingi kwenye mechi tatu mfululizo za klabu hiyo, jambo ambalo halikuwahi kutokea tangu alipojiunga na timu hiyo.

Samatta amecheza kwa dakika 261 ndani ya mechi tatu alizocheza ndani ya Genk, ambazo ni nyingi zaidi kwake kucheza tangu alipojiunga na timu hiyo na ndani yake amecheza dakika 90 katika mechi za mashindano dhidi ya Eupen na Oestende huku akifunga bao moja.

Mshambuliaji huyo aliuambia mtandao wa Genk kuwa anatambua ana kazi kubwa mbele yake na amekuwa akijitahidi kujituma mazoezini ili kuweza kufanya vizuri.