Kiggi afunga pazia Singida United

Muktasari:

Kiggi tayari yuko Mwanza kujiunga na klabu hiyo iliyoweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara chini ya kocha wake Hans Pluijm.

Dar es Salaam. Nahodha wa zamani wa Ndanda, Kiggi Makassi amejiunga na Singida United kwa mkataba wa miaka miwili.

Kiggi tayari yuko Mwanza kujiunga na klabu hiyo iliyoweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara chini ya kocha wake Hans Pluijm.

Kuondoka kwa Kiggi ni pigo lingine kwa Ndanda ambayo tayari imewapoteza wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza wakiwamo beki wake  Paul Ngalema na  kiungo Willium Lucian  'Gallas' wako mbioni kutua Lipuli ya Iringa huku beki Nassor Kapama akiwaniwa na Majimaji.

Usajili wa kiungo huyo wa zamani wa Yanga umefunga pazi la usajili la klabu la Singida United msimu huu.

 Katibu mkuu wa Singida United, Abdurahman Sima alisema usajili wa Kiggi na kipa Ally Mustapha 'Barthez' umefunga pazia lao kwa msimu huu na sasa wanaelekeza nguvu katika maandalizi ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

"Kweli tumemsajili Kiggi kwa mkataba wa miaka miwili na tayari yuko kambini Mwanza. Kwa sasa  kilichobaki ni kuipa timu maandalizi ya nguvu ili ifanye vizuri kwenye ligi," alisema Sima.

Sima alisema wamechagua kuweka kambi Mwanza kutokana na kuwa na timu nyingi zitakazowapa mazoezi mazuri yatakayowajenga wachezaji wao kwa ajili ya ligi.