Lwandamina ajivunia kikosi chake

Muktasari:

  • Kikosi hicho cha Lwandamina kitakuwa na kibarua kizito cha kutetea ubingwa wake wa Ligi  Kuu Bara kuanzia Agosti 27 itakapocheza dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Taifa.

 Kocha mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina ameanza kulidhishwa na maandalizi ya timu yake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kikosi hicho cha Lwandamina kitakuwa na kibarua kizito cha kutetea ubingwa wake wa Ligi  Kuu Bara kuanzia Agosti 27 itakapocheza dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Taifa.

Yanga ilianza maandalizi ya msimu mpya kwa kufanya mazoezi ya Gym jijini hapa kabla ya kwenda mkoani Morogoro ambapo waliendelea na mazoezi ya kujenga utimamu wa mwili kwa kukimbia na mapalashuti.

"Tumejiandaa na tunaweza kuanza ligi, ni wazi kuwa msimu huu utakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu timu nyingi zimejiandaa na hata kusajili vizuri," alisema Lwandamina.

Katika mazoezi ya leo asubuhi kwenye Uwanja wa Polisi Kurasini, kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alikuwa akitilia mkazo namna ya ukabaji.

 Yanga inajiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba utakaofanyika Agosti 23, jambo lililomfanya Nsajingwa kuwa mkali kwa makosa ya kizembe yaliyokuwa yakifanywa na mabeki wake. 

Mara zote Nsanjigwa alikuwa makali kwa makosa hayo na kulazimika kukaa na mchezaji mmoja mmoja ili kutoa maelekezo.