Mabondia kufunzwa ujasiriamali Dar

Muktasari:

Tamasha hilo lililoandaliwa na asasi zisizo za kiserikali za Mambo Safi na Yowede litafunguliwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hamphrey Polepole.

Dar es Salaam. Mabondia zaidi ya 40 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali katika tamasha la vijana, ajira, vipaji na masumbwi litakalofanyika Jumamosi na Jumapili kwenye Ukumbi wa White House, Kimara Korogwe jijini hapa.

Tamasha hilo lililoandaliwa na asasi zisizo za kiserikali za Mambo Safi na Yowede litafunguliwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hamphrey Polepole.

Msemaji wa tamasha hilo, Fabian Salvatory alisema mbali na kutoa elimu ya ujasiriamali, pia kutapigwa mapambano sita ya masumbwi kwa mabondia wanaofanya vizuri kwa sasa nchini.

“Lengo la Tamasha hili ni kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wenye vipaji,” alisema Salvatory na kuongeza.

“Maandalizi yote ya tamasha yamekamilika ikiwa ni pamoja na kuleta wakufunzi wa ujasiriamali ambao watatoa mafunzo hayo kwa vijana wetu wenye vipaji.

“Tunatarajia kuwa na mabondia 40, makocha na mashabiki wao watashiriki. Vilevile tunakaribisha mtu yoyote atakayependa kushiriki katika tamasha hili siku ya Jumamosi, hakutakuwa na kiingilio katika mafunzo hayo.

“Baada ya mafunzo, mabondia watakaozichapa watapima uzito na afya siku hiyo tayari kupanda ulingoni Jumapili,” alisema.

Kwa mujibu wa Salavatory, kwenye mapambano ya ngumi Jumapili, mashabiki watachangia Sh8,000, wakati kwenye semina ya Jumamosi hakutakuwa na uchangiaji.

Aliwataja mabondia watakaozichapa siku hiyo kuwa Mustapha Dotto na Manyi Issa, Abdallah Luwage na Shedrack Ignas, Haidar Machajo na Said Chino na Athuman Yanga na Hashimu Chisora.

Wengine ni Julius Jackson atakaetoana jasho na Emilio Norfat, Emmanuel Kisiwani atazichapa na Elisame Mbwambo na Mohamed Muhunzi akimenyana na Kassim Ahmed.