Madai ya Simba sasa yamsubiri Mvela

Muktasari:

Simba inadai kiasi hicho cha fedha wakidai Yanga ilimsajili Kessy huku wakifahamu kuwa mchezaji huyo alikuwa na mkataba nayo.

Dar es Salaam. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana jana inataraji kutoa uamuzi wa madai ya Simba ya Sh120 milioni kwa beki wake wa zamani Hassan Kessy kuidhinishwa kuichezea Yanga.

Simba inadai kiasi hicho cha fedha wakidai Yanga ilimsajili Kessy huku wakifahamu kuwa mchezaji huyo alikuwa na mkataba nayo.

Gazeti hili lilishuhudia viongozi waandamizi wa Simba, Zakaria Hanspoppe na Godfrey Nyange ‘Kaburu’ wakiingia ofisi za TFF saa 4:00 asubuhi na kukataa kuzungumza lolote.

Hanspoppe alitoka katika kikao hicho saa 8:20 mchana na hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo zaidi ya kusema kamati ndiyo yenye jukumu la kutangaza uamuzi ulioafikiwa.

“Sakata la kessy limemalizika, mimi siwezi kusema yaliyoamuliwa, kamati ndiyo itakayosema uamuzi ulioafikiwa,” alisema Hanspoppe kwa kifupi.

Awali, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Eliud Mvela alisema kamati yake itatoa uamuzi wa masuala yote yaliyofika mezani kwake baada ya kusikiliza pande zote.