Mashabiki wakamatwa, wafungiwa kwenye karandinga

Muktasari:

Licha ya TFF kueleza milango ya uwanja huo kufunguliwa saa tano asubuhi, lakini walilazimika kuifungua saa tatu asubuhi kutokana na wingi wa mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo na kuingia moja kwa moja uwanjani.

Jeshi la Polisi limetumia mbinu mbadala ya kuwakamata baadhi ya mashabiki waliokuwa wakishinikiza kuingia uwanjani licha ya kuwepo kwa amri ya mashabiki kutoingia uwanjani kufuatia majukwaa kujaa na kuamua kuwafungia katika magari ya polisi (Kalandinga)

Saa saba kamili, TFF inatoa tangazo la kueleza uwanja umejaa na hawaruhusu shabiki yeyote kuingia ndani ya uwanja licha ya ubishi wa mashabiki walioko nje ambao wanatawanywa kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha, lakini baada ya muda wanarejea tena na polisi kuamua kuwakamata na kuwafungia kwenye karandinga

Ukipotea njia imekula kwako Uwanjani

Saa tano na robo, tayari mashabiki wa Simba na Yanga walianza purukushani baada ya Yanga kumtimua shabiki wa Simba na Wakongo wawili waliopotea njia na kuibukia upande wa mashabiki wa Yanga.

Simba nayo ilijibu mapigo kwa kumsurubu shabiki wa Yanga aliyeibukia upande wa mashabiki wa Simba,

Yanga yawa wapole kwa Simba

Simba ni kama imedhamiria, kwani safari hii haitaki kuonewa na Yanga ambayo ilianza kwa 'kuibip' Simba kwa kufunga bango la njano kuzunguka jukwaa lililokaliwa na mashabiki wa Simba ambao wanaishangilia TP Mazembe.

Kitendo kile kiliibua mshikeli kwa mashabiki wa Simba ambao walianza kulivuta bango hilo na Yanga kujikuta wakiwa wapole na kulitoa kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Yanga, Mazembe haijawai tokea

Haijawahi kutokea Tanzania kwa miaka 10 iliyopita kwa mashabiki kuingia uwanjani kuanzia saa 3:00 asubuhi kwa lengo la kushuhudia mechi ya Yanga dhidi ya TP Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya TFF kueleza milango ya uwanja huo kufunguliwa saa tano asubuhi, lakini walilazimika kuifungua saa tatu asubuhi kutokana na wingi wa mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo na kuingia moja kwa moja uwanjani.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema walilazimika kufungua milango ya uwanjani mapema tofauti na walivyoeleza awali kutokana na mashabiki kufurika uwanjani kuanzia saa tatu asubuhi.

"Mashabiki walianza kumiminika uwanjani kuanzia saa tatu, hatukuwa na namna zaidi ya kufungua milango ya uwanja muda huo ili kuwapa fursa ya kuingia na kupunguza msongamano," alisema Lucas.

Kama ambavyo jeshi la Polisi liliahidi kuimarisha usalama, mapema asubuhi polisi wa vikosi mbalimbali walimiminika uwanjani hapo kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa hali ya amani na usalama.

Mashabiki Simba wawa watulivu

 

Mashabiki wa Simba nao waliwasili uwanjani mapema na kama walivyoahidi kuwa upande wa wageni wao TP Mazembe, ndivyo walivyofanya.

"Mashabiki hao walikwenda sambamba na wale wa Yanga ambao walianza kumiminika uwanjani kuanzia saa tatu asubuhi na kama walivyoahidi walipitiliza moja kwa moja kwenye majukwaa ya upande wa Mazembe huku wakiwa katika ari ya utulivu.

Neema yatinga taifa

Mchezo huo ni kama umeleta neema kwa watoa huduma ya usafirishaji, kwani magari yaliyokodishwa na mashabiki hao ni mengi na yamekuwa yakishusha abiria kila baada ya dakika chache.

Uwanja wafurika asubuhi

Hadi kufikia saa 10:40 asubuhi robo tatu ya majukwaa ya uwanja yalikuwa yamejaa ambapo kwa mujibu wa timu ya Mwananchi iliyopiga kambi Taifa, kama hali itaendelea hivyo hadi kufikia saa sita mchana uwanja utakuwa umejaa.

Magari ya maji ya kuwasha yaongezwa

Kama ambavyo kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alivyoahidi, jeshi la Polisi linaonekana kujipanga kukabiliana na yeyote atakayefanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuongeza idadi ya magari ya kuwasha ambayo katika mchezo wa leo yameletwa matano.

Mashabiki wazuiwa kuingia uwanjani

Hadi kufikia saa 11:53 asubuhi, mashabiki waliokuwa nje ya uwanja hawakuruhusiwa kuingia ndani baada ya uwanja kujaa na nafasi ya kuingia uwanjani imebaki kwa watu maalumu na Wanahabari pekee.

Kitendo cha kuzuiwa huko mashabiki walilazimisha na kuvunja geti jambo lililosababisha polisi kutumia mabomu ya machozi, na maji ya kuwasha ili kuwatanya uwanjani hapo.

Mashabiki wavunja geti taifa

Baada ya kuzuiliwa na TFF kuwataka askari kutoruhusu shabiki yoyote kuingia uwanjani, hali imekuwa tete baada ya mashabiki kuvunja geti lililopo nyuma ya majukwaa yaliyokaliwa na mashabiki wa Simba na kuingia uwanjani huku askari wakionekana kuelemewa na wingi wa mashabiki.

Kwa mujibu wa ripota wetu, Ibrahim Bakari, jeshi la polisi limeongeza nguvu kwa kuongeza idadi ya askari ili kuhakikisha usalama katika mchezo huo wa Shirikisho barani Afrika.

Tayari polisi wameanza kuwadhibiti mashabiki wanaoshinikiza kuingia uwanjani kwa kupiga mabomu ya machozi na kutumia maji ya kuwasha kuwatawanya baada ya kuzuiwa kuingia kutokana na uwanja kujaa huku mashabiki hao wakifanya ubishi na kutaka kuingia kwa nguvu.

FFU 50 waingia ndani ya uwanja

Dakika chache baada ya mashabiki wa Simba na Yanga kuanza tafrani, askari wa kutuliza ghasia (FFU) kama 50 wanaingia uwanjani wakiongozwa na Mkuu wa Usalama wa viwanja, Hashimu Abdallah ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji wa Yanga.

Mashabiki wa Yanga wanawashangilia askari hao, wanapewa maelekezo na kujipanga kila kona ya uwanja huo huku wakiwatazama mashabiki.