Maximo aahidi neema

Kocha wa Yanga, Marcio Maximo.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Wachezaji wa Yanga hawapewi posho za mazoezi baada ya viongozi wa Yanga kudai nyota hao wanalipwa mishahara mikubwa tofauti na timu nyingine.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Marcio Maximo amewatoa hofu nyota wake kwa kuwaahidi kupigania masilahi mazuri kwa kila mmoja, wakati wachezaji hao wakisotea mishahara yao ya mwezi uliopita.

Maximo aliwaambia wachezaji wake baada ya mazoezi ya juzi asubuhi kwenye Uwanja wa Loyola jijini Dar es Salaam kuwa yeye ni mmoja wa watu wanaopigania masilahi ya wachezaji na wiki iliyopita alikutana na mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuph Manji na kuzungumza naye kuhusu jambo hilo hivyo amewataka wachezaji wake wacheze mpira  na kuhusu masilahi wasiwe na shaka.

“Nimekuwa nikipigania masilahi mazuri ya wachezaji tangu nikiwa  na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na nataka kufanya hivyo hata nikiwa hapa, lakini muhimu ni kunihakikishia kuwa mtajituma uwanjani na  kujitolea na mnithibitishie hilo.

“Nimeongea na Manji kuhusu jambo hilo na msiwe na wasiwasi kila mmoja wenu atapata masilahi mazuri na kufurahia soka, lakini hakikisheni mnajituma uwanjani na kufanya vizuri na ndipo kila kitu kitakwenda vizuri upande wenu,” alisema Maximo.

Hata hivyo; licha ya Maximo kutoa tumaini hilo kwa wachezaji wake, lakini upande wa pili wachezaji hao wamelalamikia kutopata mishahara yao ya mwezi uliopita mpaka sasa jambo ambalo linawaweka katika wakati mgumu katika mazoezi yao.

Wachezaji hao wamedai kuwa wanategemea mshahara huo kwa ajili ya kujikimu mahitaji mbalimbali kama chakula  na usafiri, lakini wanashangazwa na ukimya wa viongozi wao hadi sasa.

“Ukweli hali ni mbaya tunafanya tu mazoezi kwa kuwaheshimu viongozi, lakini wengi hatuna fedha na hatujui tutapata lini na kama unavyojua tunategemea mshahara kwa ajili ya chakula na usafiri, na mazoezi yenyewe magumu  sasa hata hatujui tutaishije halafu ni bora hata tungekuwa tunapata posho, basi mshahara tusingekuwa na haja nao lakini hakuna kitu tunachopata,” walidai wachezaji hao huku wakiombwa wasiandikwe majina yao gazetini.

Gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu ajibu malalmiko hayo lakini simu yake iliita bila ya majibu na baadaye ikazimwa kabisa.

Inadaiwa kuwa nyota wa timu hiyo wakiongozwa na Mrisho Ngasa na Mbuyu Twite mara nyingine hawatokei katika mazoezi hayo na hata wakitokea wamekuwa wakifanya chini ya kiwango kutokana na jambo hilo la kutopata mshahara kuwaumiza.

Juzi katika mazoezi yaliyofanyika Loyola wachezaji hao hawakutokea huku kocha wao  Maximo aking’aka  kwani hawakumpa taarifa zao  za kukacha mazoezi na wala hawakutoa taarifa yoyote kwa viongozi.

Wachezaji wa Yanga hawapewi posho za mazoezi baada ya viongozi wa Yanga kudai nyota hao wanalipwa mishahara mikubwa tofauti na timu nyingine.

Kwa sasa Azam ndiyo inayolipa wachezaji wake mishahara mikubwa ikifuatiwa na Yanga na Simba inashika nafasi ya tatu.