Monday, March 20, 2017

Murshid asema kazi imeanza Msimbazi

 

By Oliver Albert,Mwananchi

Dar es Salaam. Beki wa Simba,Juuko Murshid amefurahia kurejea tena kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kudai kuwa ataendelea kujituma ili aweze kucheza kila mara kutokana na ushindani uliopo katika nafasi  hiyo hizi sasa.

Mchezaji huyo alirejea kikosi cha kwanza juzi katika mchezo wa Kombe la Shirikisho(FA) dhidi ya Madini ya Arusha uliomalizika kwa Simba kushinda bao 1-0.

Juuko aliingia katika mgogoro na viongozi wake baada ya kuchelewa kujiunga na kikosi hicho kutokana na kupata ruhusa ya kurejea Uganda  ili kuitumikia timu yake ya Taifa katika mashindano ya Mataifa ya Afrika yaliyofanyika Januri nchini Gabon.

Kutokana na beki huyo kuchelewa kocha wa Simba, Joseph Omog ilibidi amchezeshe kiungo Abdi Banda kama beki wa kati nafasi ambayo ameonekana kuimudu akicheza sambamba na Method Mwanjali wakati mwingine Novalt Lufunga.

Kuchelewa kurejea kwa beki huyo kuliwapa wakati mgumu Simba baada Mwanjali kuumia huku Lufunga akionekana kutocheza vizuri hivyo kumlazimu Omog kumchezesha kiungo James Kotei au beki wa pembeni,Janvier Bokungu kucheza pamoja na Abdi Banda.

Jambo hilo lilifanya Simba kuyumba katika mechi za karibuni na kuamsha hasira kwa mashabiki waliotaka Juuko arejeshwe haraka kikosini kwani haiwezekani beki anayecheza kikosi cha kwanza katika taifa lake aanzie benchi katika klabu.

-->