Monday, June 19, 2017

Mwamanda ampa tano Mayay kwa kuamuzi wa kugombea urais wa TFF

 

By Fredrick Nwaka, Mwananchi fnwaka@mwananchi.co.tz

Wakati hekaheka za wadau kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa TFF zikipamba moto, beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars Samson Mwamanda amesema anamuunga mkono Ally Mayay kugombea urais.

Mayay amechukua fomu ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika Agosti 12 mkoani Dodoma.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mwamanda alisema umefika wakati wachezaji wa mpira wakajitosa kuwania nafasi za uongozi wa soka ili kuuokoa mpira wa Tanzania.

“Ally Mayay ni mtu jasiri, sijashangazwa na uamuzi wake wa kugombea, ameuishi mpira wa Tanzania na anajua wapi unatakiwa kwenda. Viongozi wengi waliopo TFF wako kwa ajili ya matumbo yao na si maendeleo ya soka,”alisema Mwamamnda aliyewahi kuichezea Prisons.

Wakati huohuo, mchezaji huyo amesema anatarajia kuchukua fomu ya kuwania ujumbe wa kanda ya Dar es Salaam katika uchaguzi mkuu ujao.

 

-->