Nyota wa Serengeti Boys wapata shavu Ligi Kuu

Nyota wa Serengeti Boys, Nickson Kibabage (kulia) akimtoka beki wa Niger, Ibrahim Namata katika mechi ya AFCON 2017 Mei mwaka huu nchini Gabon. Kibabage anachezea Mtibwa. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Serengeti Boys iliondoshwa katika mashindano ya vijana chini ya miaki 17 yaliyofanyika Gabon Mei 4 hadi 28 kwa kanuni ya uwiano wa matokeo baina yao baada ya kulingana pointi na Niger (pointi nne).

Dar es Salaam. Baadhi ya vijana waliounda kikosi cha Serengeti Boys, wamesajiliwa timu za Ligi Kuu msimu huu na kocha aliyekiongoza kikosi hicho, Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ amezitaka timu hizo kuwatumia vizuri vijana hao.

Serengeti Boys iliondoshwa katika mashindano ya vijana chini ya miaki 17 yaliyofanyika Gabon Mei 4 hadi 28 kwa kanuni ya uwiano wa matokeo baina yao baada ya kulingana pointi na Niger (pointi nne).

Miongoni mwa wachezaji wa Serengeti Boys watakaoshuhudiwa msimu ujao Ligi Kuu Tanzania Bara ni mlinzi Dickson Job aliyesajiliwa Mtibwa Sugar na kipa Ramadhan Kabwili na Said Mussa waliokwenda Yanga.

Waliopata nafasi ya kucheza Ligi Kuu, yupo Yohana Mkomola ambaye muda wowote anaweza kujiunga na Étoile Sportive du Sahel ya Tunisia.

Mlinzi wa kati Job ambaye amepandishwa katika kikosi cha kwanza Mtibwa Sugar ameonekana kufurahia nafasi hiyo na kupandishwa kwake kumechangiwa na mashindano ya vijana.

Baada ya kurejea nchini wadau walizua maneno mengi huku wengi wao wakihoji mipango kwa vijana ambao walionyesha kiwango bora katika mashindano licha ya kuondolewa katika hatua ya makundi.

“Kuendesha timu na mipango kwa ujumla ya maendeleo ya soka la vijana ni gharama kubwa, baada ya kurejea kutoka katika mashindano kumekuwa na mapumziko kwa vijana ili baadaye waje kuunda kikosi cha Ngorongoro Heroes.

“Lakini katika mapumziko hayo kuna anayejua wanachokifanya mitaani? Swali gumu hilo ambalo siwezi kulijibu kama ukiniuliza, tunaweza kushirikiana na timu zetu ili vijana wetu kuendelea kuwa katika mazingira mazuri ya soka,” alisema Shime.

“Pongezi zangu ziende kwa timu zilizoamua kuwasajili vijana wa Serengeti Boys, unaposajili kijana ina maana kuwa unatusaidia malezi ya kijana kuendelea kuwa katika misingi bora ya soka.

Hata hivyo, kocha huyo alizitaka timu hizo kuwatumia vizuri vijana hao maana bado wanafundishika kutokana na udogo wao kiumri.

Shime alizungumzia pia mazingira ya Kitanzania na kuwatolea uvivu wale wanaodai kuwa vijana hao wanaweza kupotea katika medani ya soka kama watazichezea timu za nyumbani.

“Wangepata nafasi ya kuchezea Ulaya moja kwa moja ingekuwa nzuri na ingependeza maana wangekulia katika misingi bora zaidi ya soka kuliko hapa nyumbani, kuna muda inabidi tuishi kwa kuzingatia mazingira yetu namna yalivyo.

Job alisema: “Hii ni nafasi kwangu kuendelea kuonyesha uwezo wangu, kukua kwa kiwango changu kumechangiwa na kikosi cha Serengeti Boys.

“Mashindano yale yamenijenga na kuona hakuna kinachoshindikana hata kama umri wangu ni mdogo, lakini nina nafasi ya kupigania namba katika kikosi cha kwanza cha Mtibwa Sugar.”

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubeir Katwila alisema kijana wake, Job ameonekana kukomaa na kwa taratibu za timu yao ilibidi apandishwe kwa ajili ya kumuendeleza kisoka.

“Wengi wanajua Mtibwa huwa ina utaratibu wa kuwatumia vijana wake na hata kupandishwa kwa Job sio jambo geni,” alisema.

“Muhimu kwake ni kuzingatia maelekezo na kujifunza falsafa ya timu kikamilifu.”