Profile yaanza kutetea ubingwa wake

Muktasari:

  • Mchezo huo ambao ulikuwa mkali kwa timu hizo kusaka ushindi kwenye mechi hiyo ya kwanza, Profile ilijikuta ikitembeza mkong’oto kwa wapinzani wao na kuondoka vifua mbele.

Mwanza. Mabingwa watetezi wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza, Profile wameanza vyema ligi hiyo kwa kuitandika Worriors kwa pointi 70-57 katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa BOT Pasiansi jijini hapa.

Mchezo huo ambao ulikuwa mkali kwa timu hizo kusaka ushindi kwenye mechi hiyo ya kwanza, Profile ilijikuta ikitembeza mkong’oto kwa wapinzani wao na kuondoka vifua mbele.

Nyota katika mchezo huo kwa Profile walikuwa Shaban Ally aliyevuna pointi 25, Mwasalile Mpnjoli (23) na Lugina Lamabrt (13) na kuifanya timu yao kuibuka na ushindi.

Nahodha wa Profile, Mwasalile Mponjoli alisema ushindi huo wa kwanza unawapa hamasa na kujigamba kutwaa ubingwa kwa mara nyingine.

Mponjoli alisema kama walivyoahidi kutetea ubingwa wao msimu huu, hawaoni timu yoyote itakayowaharibia mipango yao kutokana na namna walivyojipanga.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliopigwa majira ya saa 10 alasiri, Kisesa iliichapa Hawks kwa pointi 38-31, mchezo ambao ulikuwa wa ushindani.

Mratibu wa ligi hiyo, Haidari Abdul alizitaka timu kujiandaa vyema ili bingwa atakayepita aweze kuuwakilisha Mkoa vizuri na kwa mafanikio.

"Kwanza niwaombe wadau wajitokeze kwa wingi viwanjani kuwashangilia wachezaji, lakini pia niziombe hizi timu zijipange kiushindani kwa sababu Ligi ya Mabingwa ni ngumu kwahiyo tunataka timu bora," alisema Abdul.