Ronaldo amnunia Zidane, Real ikilazimishwa sare

Muktasari:

Ni mara ya kwanza kwa mshambuliaji huyo kutomaliza dakika 90 za mchezo

Madrid, Hispania. Mshambuliaji Cristiano Ronaldo alimnunia bosi wake, Zinedine Zidane wakati Real Madrid ikilazimishwa sare 2-2 na Las Palmas juzi.

Bao la dakika za majeruhi la Sergio Araujo lilitosha kuwaduwaza vinara hao wa La Liga muda mfupi baada ya Ronaldo kupumzishwa.

Katika mchezo huo, Real Madrid iliongoza kwa kufunga mabao mawili ya mapema, lakini Las Palmas ilisawazisha mabao yote na kuwafanya mabingwa hao mara 11 wa Ulaya kuambulia sare ya pili mfululizo.

Tukio la Ronaldo kupumzishwa lilionekana kumkera wakati akitoka uwanjani dakika ya 72 ya mchezo huo ikiwa ni mara yake ya kwanza katika maisha yake ya soka akiwa Real Madrid.

Ronaldo alionekana akifoka kwa hasira baada ya kocha wake, Zinedine Zidane kuamua kumpumzisha.

Alieleza baada ya mchezo huo kushangazwa na uamuzi wa kocha wake kumtoa dakika ya 72, akieleza kuwa kwa miaka saba hajawahi kuona tukio kama hilo, uamuzi ambao Zidane aliueleza kuwa ulikuwa kwa sababu za kiufundi.

Zidane alimpa mkono Ronaldo wakati akitoka uwanjani, ambao aliupokea bila kumtazama usoni bosi wake.

Hata hivyo, uamuzi huo ulionekana kuwa hasara kwa Real Madrid baada ya mchezaji wa zamani wa kikosi cha pili cha Barcelona, Sergio Araujo kufunga bao la kusawazisha dakika na matokeo kuwa 2-2.

Timu hiyo kutoka kisiwa cha Canary imeanza vyema msimu wa Ligi Kuu Hispania na mara mbili iliwazuia vijana hao wa Zidane kwa kurejesha mabao yao.

Kocha huyo, raia wa Ufaransa alimpumzisha Ronaldo zikiwa zimebaki dakika 18 mchezo huo kumaliza, uamuzi ambao ulizua utata.

Muda mfupi baadaye, Araujo mwenye miaka 24, raia wa Argentina aliyewahi kucheza kikosi B cha Barca B kwa mkopo msimu wa 2012-13 aliisawazashia timu yake.

Aliwazidi mbinu mabeki wa Real Madrid na kumtungua kipa Kiko Casilla baada ya kosa la beki Nacho kushindwa kuokoa mpira kwenye mstari.

Udhaifu wa safu ya ulinzi ya Real Madrid uliiwezesha Las Palmas kuondoka na pointi moja muhimu katika mchezo huo.