Monday, March 20, 2017

Simba, Madini wavunja rekodi ya mapato Arusha

 

By Yohana Challe, Mwananchi

Arusha. Mchezo wa robo fainali baina ya Simba na Madini Sc uliopigwa juzi uwanja wa Sheikh Amri Abeid na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, umevunja rekodi ya mapato ya zaidi ya milioni 80.

Taarifa ya Chama cha Soka mkoa wa Arusha imesema uwanja huo unabeba idadi ya mashabiki 12,000, lakini juzi uliingiza watu 14,056 kwa waliokata tiketi pekee huku wengine wakizuiwa kuingia kutokana na sababu za kiusalama, kwani uwanja ulijaa kuzidi uwezo licha kuwa walikuwa na tiketi mkononi.

Mgawo wa mapato ya mchezo huo, Serikali ilifaidika kupitia kodi VAT Baada ya kupata Sh12,421,067, wamiliki wa uwanja ambao ni CCM walipata Sh9,678289, timu ya Madini SC ilipata Sh16,130,483 sawa na Simba.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Sh12,904,386, Chama cha soka mkoa wa Arusha (ARFA), Sh3,226,096,huku gharama za mchezo zikiwa ni Sh6,452,193,na kufanya jumla ya Sh81,427,000 kwa idadi ya watazamaji 14,056.

Mapato hayo hayajawahi kutokea kwenye uwanja huo wa Sheikh Amri Abeid tangu mwaka 1976 wakati Pan African ilipovaana na timu ya Vita kutoka Zaire.

Hata hivyo, Katibu wa siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe, alisema kuwa kuna uharibifu wa mageti ulijitokeza kwenye mchezo huo na tayari watatumia mapato hayo kufanya ukarabati.

“Baada ya ligi ya mkoa kumalizika, tutaufunga uwanja huu kwa muda usiojulikana, ili kufanya ukarabati uwanja mzima kuanzia majukwaa, vyumba na hata nyasi za uwanja,” amesema Mdoe.

Aliongeza kuwa suala la kuufunga uwanja lilikuwa tangu mwezi uliopita japo ARFA iliomba zoezi hili lisitishwe ili ligi daraja la tatu ngazi ya Mkoa imalizike ndipo mambo menine yaendelee.

-->