Simba yapeta, Kiluvya yaduwaza

Muktasari:

Wakati Simba iliyoshinda kwa mabao 2-0 ikiungana na Prisons na Toto African kusonga mbele, matokeo ya kushangaza yalitokea kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandinzi wakati timu ya daraja la kwanza, Kiluvya United ikiichapa Ruvu Shooting inayoshiriki Ligi Kuu kwa mabao 2-1 na kuwatupa nje ya mashindano hayo.

Dar/Mikoani. Mabao ya Pastory Athanas na Mohammed Hussen ndiyo jambo pekee lililoonyesha tofauti kati ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba na Polisi Dar katika mchezo wa Kombe la FA uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Wakati Simba iliyoshinda kwa mabao 2-0 ikiungana na Prisons na Toto African kusonga mbele, matokeo ya kushangaza yalitokea kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandinzi wakati timu ya daraja la kwanza, Kiluvya United ikiichapa Ruvu Shooting inayoshiriki Ligi Kuu kwa mabao 2-1 na kuwatupa nje ya mashindano hayo.

Dar es Salaam. Pamoja na kuonyesha mpira wa ovyo mbele ya mashabiki wake Simba ilifanikiwa kupata bao la mapema lililofungwa na Athanas katika dakika ya tatu ya mchezo akimalizia pasi nzuri ya Shiza Kichuya.

Dakika ya 82, Mohammed Hussein aliipatia Simba bao la pili akimalizia kwa kichwa mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kutokana na shuti alilopiga mwenyewe.

Zaidi ya mabao hayo, timu zote mbili zilishindwa kuonyesha mipango na soka la kuvutia licha kukosa nafasi kadhaa.

Kocha msaidizi wa Simba, Iddi Salim alisema kuwa wapinzani wao walikuwa bora uwanjani, jambo lililowapa wakati mgumu.

 “Tuliutumia mchezo huu kama kipimo kuelekea mechi yetu dhidi ya Azam FC wikiendi ijayo. Mechi haikuwa rahisi na wapinzani wetu walionyesha kiwango bora.

“Siku zote siyo kazi nyepesi kucheza na timu kama hizi, lakini jambo la muhimu ni kuwa tumepata ushindi na kusonga mbele,” alisema Salim aliyewahi kufanya kazi Gor Mahia ya Kenya.

Kocha wa Polisi Dar, Ngero Nyanjaba alisema kuwa timu yake imepoteza mechi kutokana na wachezaji wake kukosa umakini.

“Tulipata nafasi nyingi nzuri tukashindwa kuzitumia lakini wenzetu walitumia uzoefu wa kutumia nafasi zao chache walizopata wakaweza kufunga mabao yaliyowapa ushindi,” alisema Nyanjaba.

Mbeya. Prisons imeitambia Mbeya Warriors kwa kuitandika mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Prisons ilipata mabao yake mawili kupitia kwa Emmanuel Mnyali na Mohamed Samatta wakati  Mbeya Warriors ilipata bao la kufutia machozi lililofungwa kwa penalti iliyopigwa na Eliuter Mpepo baada ya beki wa Prison, James Mwasote kushika mpira katika eneo la hatari.

Mwanza. Toto African imetumia vizuri uwanja wake wa nyumbani kwa kuichapa Mwadui kwa penalti 5-4 baada ya kutoka sare mabao 2-2 kwenye Uwanja CCM Kirumba, Mwanza.

Toto ilipata mabao yake kupitia kwa  Mohamed Soud na Hamim Abdul kabla ya Mwadui kusawazisha baada ya beki wa Toto, Yusuph Mlipili kujifunga mwenyewe wakati akimrudishia mpira kipa wake David Robert mpira uliokwenda moja kwa moja wavuni huku bao la pili likifungwa na Salum Amis.

Imeandaliwa na Charles Abel (Dar es Salaam), Saddam Sadick (Mwanza), Godfrey Kahango (Mbeya)