Ufungaji Simba wamtesa Omog

Kocha wa Simba, Joseph Omog

Muktasari:

  • Simba itapambana na Azam Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara. Mara ya mwisho timu hizo kukutana ni kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar na wekundu hao wa Msimbazi kulala kwa bao 1-0.

Dar es Salaam.Kocha wa Simba, Joseph Omog ni kama amesikia kelele za mashabiki wa klabu hiyo ambao wanasononeka na kiwango duni cha safu yao ya ushambuliaji na ametamka kuwa wiki hii atadili nayo ikiwa ni maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Azam Jumamosi.

Simba itapambana na Azam Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara. Mara ya mwisho timu hizo kukutana ni kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar na wekundu hao wa Msimbazi kulala kwa bao 1-0.

Omog alisema katika mazoezi ya wiki hii ni mwendo wa kuwanyoosha washambuliaji wake, kwani ametambua kuwa ndiyo sehemu pekee ambayo haiko vizuri ndani ya kikosi chake.

Safu ya ushambuliaji ya Simba imekuwa butu kwenye Ligi Kuu Bara na haijafunga bao lolote tangu Oktoba mwaka jana, huku mabao manne ya timu hiyo yaliyofungwa kwenye mechi nne za mzunguko wa pili yakifungwa na viungo.