Monday, March 20, 2017

Viongozi wa ZFA waanza kujipanga

 

By Haji Mtumwa,Mwananchi

Zanzibar. Siku chache baada ya Zanzibar kupatiwa uanachama wa kudumu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF),Rais wa Chama cha Mpira wa miguu Zanzibar, Ravia Idarous Faina  amekutana na Wenyeviti na Makatibu  wa chama hicho kutoka  wilaya saba za Ungujan ili kuwapa muongozo wa mifumo ya uongozi.

Ravia amelazimika kukutana na viongozi hao wa soka wilayani kwa lengo la kuwapatia taarifa kuhusiana na mifumo ya uongozi wa soka inavyotakiwa kuwepo hivi sasa hususa suala la mfumo wa ligi daraja la pili wilaya.

Moja ya maagizo waliyopewa ZFA na CAF ni kuanza kupunguza klabu Wilayani kwa upande wa daraja la Pili zikitakiwa timu zisiyozidi 20. 

Katibu wa ZFA wilaya ya Kaskazini A, Msellem Haji amezungumza kwa niaba ya viongozi hao ambapo amesema wakati Zanzibar imepatiwa fursa ya kuwa mwanachama wa Shirikisho hilo barani Afrika hakuna pingamizi juu ya kufumua mfumo wa ligi.

"Kwa niaba ya makatibu wa ZFA Wilaya za Unguja tumekubali kuyafuata maagizo tuliyopewa mana tumetakiwa daraja la pili timu zisizidi 20, hivyo kuanzia sasa inatubidi tufumue mfumo na tucheze ligi ndogo na timu zibakie 16 na nne zitakazopanda ili ziwe 20 kwa msimu ujao," amesema Msellem.

-->