Yanga kuibukia kwa Toto, Azam kwa Mtibwa

Kocha wa Yanga ,Hans Pliujm

Dar es Salaam. Baada ya kuonyesha kiwango duni dhidi ya Azam, Yanga leo ina uhakika wa kuwafurahisha mashabiki wake itakapoivaa Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Wakati Yanga ikijifariji, Azam iliyotoka sare 0-0 na Yanga, Jumapili itaikabili Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Yanga inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 15, haijawahi kupoteza dhidi ya Toto katika miaka mitano waliyokutana Ligi Kuu.

Timu hiyo inayo nafasi ya kushinda kirahisi dhidi ya Toto kutokana na historia ya udugu baina ya timu hizo. Msimu uliopita mabingwa hao mara 26 walishinda mechi zote mbili kwa mabao 4-1 na 2-1.

Mwenendo mbovu wa Toto msimu huu ikiwa imepoteza mechi nyingi kwenye uwanja wake wa nyumbani na ugenini, unaweza kuibeba Yanga. Mjadala umeibuka miongoni mwa mashabiki, baadhi yao wakitetea kuwa uchovu wa kutopumzika kwa wachezaji wa kikosi hicho tangu kumalizika kwa ligi msimu uliopita umechangia kuonyesha kiwango duni uwanjani wakati wengine wakidai uwezo wa kocha Hans Pluijm na benchi lake la ufundi umeshuka.

Suluhu dhidi ya Azam imewatia hasira mashabiki ambao wanashinikiza Pluijm awapumzisha wachezaji na kuwapa nafasi wengine, huku mshambuliaji Donald Ngoma akiwa ni mmoja wa wanaotakiwa kupigwa benchi kwa madai kuwa amechoka na hana msaada.

Mashabiki wanamtaka kiungo, Haruna Niyonzima aanze kikosi cha kwanza ili kusaidiana na Thabani Kamusoko na kuirejeshea kasi timu hiyo. Hata hivyo, uamuzi unabaki kuwa wa kocha.

Vita kali Chamazi

Azam iliyopoteza mwelekeo na makali yake msimu huu, itakuwa na kibarua mbele ya Mtibwa Sugar mchezo utakoanza saa moja usiku.

Timu hiyo tajiri imekuwa na mwenendo wa kusuasua baada ya kupata matokeo yasiyoridhisha katika michezo mitano iliyopita.

Kocha Zeben Hernandez ameendelea kuilaumu safu yake ya ushambuliaji kuwa ndiyo inayomwangusha akiahidi kuiboresha Novemba wakati wa usajili wa dirisha dogo.

Wakati huohuo: Kagera Sugar imepanda hadi nafasi ya tatu kwa muda baada ya kuichapa JKT Ruvu kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mabatini. Bao pekee la Kagera lilifungwa na Mbaraka Yusuph dakika 87.