Yanga yawafuta machozi mashabiki wake

Kikosi cha Yanga kinachoshiriki michuano ya Shirikisho la CAF

Muktasari:

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Yanga ilifuta mkosi wa kufanya vibaya kwenye mashindano hayo, kulinda heshima yake nyumbani na kulipa kisasi kwa MO Bejaia iliyoshinda kwa bao 1-0 katika mechi ya ufunguzi ya Kundi A nchini Algeria.

Dar es Salaam.Walikuwa wapi? Ndilo swali unaloweza kuwauliza wachezaji wa Yanga baada ya kucheza kwa nidhamu na kuilaza MO Bejaia ya Algeria kwa bao 1-0 katika mchezo wa raundi ya tano wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Yanga ilifuta mkosi wa kufanya vibaya kwenye mashindano hayo, kulinda heshima yake nyumbani na kulipa kisasi kwa MO Bejaia iliyoshinda kwa bao 1-0 katika mechi ya ufunguzi ya Kundi A nchini Algeria.

Kivutio kwenye mchezo huo kilikuwa kwa mshambuliaji Amissi Tambwe aliyeifungia timu yao bao hilo katika dakika ya pili baada ya mpira wa adhabu uliopigwa vizuri na beki Juma Abdul kupanguliwa vibaya na kipa na baadaye kumgonga beki kabla ya kiwenda miguuni mwa mshambuliaji huyo Mrundi.

Hilo ni bao la kwanza la mshambuliaji huyo kwenye mechi za kimataifa msimu huu.

Kwa ushindi huo wa kwanza kwenye kundi lake, Yanga imefikisha pointi nne kenye kundi lake. TP Mazembe imeshafuzu baada ya kukusanya pointi tisa ikifuatiwa na MO Bejaia na Medeama zenye pointi tano.

Kwa maana hiyo, Yanga sasa itakuwa TP Mazembe waishinde Mediama leo na katika mchezo wa mwisho timu hiyo ya Ghana itoke sare na Mo Bejaia huku Yanga ikishinda ugenini dhidi ya wababe hao wa Congo.

Jana, kiwango bora kilichoonyeshwa na kipa Deogratius Munishi “Dida” na beki Vicent Boussou vilichangia ushindi huo ambao ulipunguziwa raha na Obrey Chirwa na Simon Msuva kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi.

“Nina furaha kwamba tumeshinda mchezo wa leo,” alisema kocha wa Yanga, Hans Pluijm baada ya mchezo.

“Mabeki wamefanya kazi nzuri ya kuzuia mashambulizi.”

Kocha huyo alilazimika kufanya mabadiliko mapema baada ya beki chipukizi wa kati, Andrew Vicent Dante kuumia na baadaye beki wa pembeni, Juma Abdul pia kuumia katika kipindi cha pili.

Nafasi ya Dante ilichukuliwa na Kelvin Yondani, ambaye katika dakika ya 74 alionyeshwa kadi ya njano itakayomfanya akose mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe.

Mejaia ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, lakini Yanga ilitengeneza nafasi za wazi kila ilipoenda golini mwa Walgeria hao. Kama wangekuwa  makini, Tambwe, Simon Msuva na hasa Chirwa, wangeweza kuongeza mabao dakika za 37 na 43, huku Mzambia huyo akipoteza nafasi dakika za 43, 68 na 84.

MO Bejaia walipata nafasi mbili lakini Soufiane Baouali na Kamel Yesli whawakuzitumia vizuri.

KWinga wa kushoto, Deus Kaseke hakuwa kwenye kiwango chake kizuri na akabadilishwa katika dakika ya 64 na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mahadhi.

Yanga

Dida; Abdul/Said Makapu, Haji Mwinyi, Dante/Yondani, Boussou; Mbuyu Twite, Msuva, Kaseke/Juma Mahadhi; Tambwe na Obrey Chirwa.

MO Bejaia

Chamsedine Rahman; Ismail BenetTayeb, Faouzi Rahal, Soufiane Khadir, Soumaila Sidibe, Zakaria Bencherifa, Mohammed Yassine, Morgan Betorangal, Baouali, Amar Benmelouka na Kamel Yesli.