Mkutano Mkuu CCM waanza ‘kimyakimya’

Muktasari:

  • Wakati idadi ya wapambe ikiwa ndogo tofauti na miaka iliyopita, hata wajumbe wanaowania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) nao walionekana wachache, huku wakitumia zaidi mitandao ya kijamii kujinadi.

Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliobeba ajenda kuu ya kukamilisha uchaguzi wa ndani wa chama hicho unaanza leo bila kuwa na shamrashamra zilizozoeleka katika mikutano iliyopita.

Wakati idadi ya wapambe ikiwa ndogo tofauti na miaka iliyopita, hata wajumbe wanaowania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) nao walionekana wachache, huku wakitumia zaidi mitandao ya kijamii kujinadi.

Ilizoeleka kushuhudia chaguzi za Taifa za chama hicho wapambe kuonekana wakibeba mabango ya CCM yenye picha za wanaowaunga mkono, huku wengine wakikusanyika karibu na kumbi za mikutano, kushindana kwa nyimbo za kuwauza wagombea wao jambo ambalo liliamsha shamrashamra katika mji wa Dodoma.

Mkutano huo unafanyika kwa siku mbili mfululizo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete.

Jana, kama ilivyokuwa kwa chaguzi za jumuiya tatu za chama hicho; Wazazi, UWT na UVCCM, wagombea wachache walionekana wakiomba kura nje ya jengo la makao makuu ya chama hicho, maarufu kama White House.

Jengo hilo lilitenganishwa kwa mageti maalumu ya kuhama na kuwekwa mashine za ukaguzi kwa yeyote aliyekuwa akiingia ndani ya viwanja hivyo.

Walioruhusiwa kuingia walikuwa ni wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Halmashauri Kuu, maofisa wachache wa chama hicho na viongozi wa Serikali.

Wafanyabiashara wanaouza sare za chama hicho na vitu vingine vidogovidogo pembezoni mwa ukuta wa jengo hilo waliondolewa hadi vikao hivyo vilipomalizika na viongozi kuondoka saa sita mchana. Uwepo wa hali ni tofauti kwa vikao hivyo na vingine na hasa kipindi cha uchaguzi, kwa kuwa nje ya ukumbi hupambwa kwa sare za chama ambazo huuzwa na wafanyabiashara.

Katika migahawa iliyopo karibu na eneo hilo kulikuwa na watu wachache tofauti na miaka mingine ya uchaguzi, ambapo watu wengi hukaa wakinywa na kula wakati wakiendelea kusubiria vikao vya utangulizi.

Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo kutoka mkoani Tanga, Asha Mohammed alilalamikia uchache wa watu.

“Wamesema tutoke kwa ajili ya usalama, lakini hata biashara hakuna na hatujui tunaishije maana tulizoea kuja na kuuza lakini watu ni wachache, hatujui waliko,” alisema Asha.

Mfanyabiashara huyo ambaye amekuwa akifika Dodoma kuuza sare za CCM kwa miaka 12, alisema hakuna wakati ambao amewahi kupata hasara kama mkutano huu.

Mtumishi wa siku nyingi wa idara ya masjala wa chama hicho aliyekataa kuandikwa jina gazetini alisema huo utakuwa ni utaratibu wa siku zote kwa kuwa CCM inahitaji kupata wanachama wenye uchungu nayo kuliko ilivyokuwa awali, ambapo wengi walipatikana kwa kelele ndani ya jengo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kumalizika vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alisema vikao hivyo baada ya kutafakari vimewapitisha kwa kauli moja Dk John Magufuli kugombea nafasi ya uenyekiti na Dk Ali Mohamed Shein kwa nafasi ya makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Alisema kwa upande wa Tanzania Bara, CCM imempitisha Philip Mangula kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti, nafasi ambayo anaitumikia hadi sasa.

“Ifahamike kwa nafasi hizi tatu za juu haziombwi kwa kujaza fomu bali hupendekezwa kwa kufanyika tathmini kwa wanachama waadilifu, waaminifu, wachapa kazi, watu ambao wamejitoa kwelikweli, watu ambao Watanzania wanawafahamu kwa mienendo yao,” alisema.

Alisema wanachama 51 wamejitokeza kuwania nafasi 15 za ujumbe wa NEC Tanzania Bara.

Polepole alisema wajumbe 1,871 wamepewa taarifa, vitambulisho na malazi yameandaliwa kwa ajili ya ushiriki wao katika mkutano huo utakaomalizika kesho.