Mkuu wa kitengo cha ununuzi Muhas asimamishwa kazi

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako 

Muktasari:

  • Pamoja na mkuu huyo wa kitengo, Profesa Ndalichako pia aliagiza kuchunguzwa kwa watu wote watakaohusika katika sakata hilo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameagiza kusimamishwa kazi kwa mkuu wa kitengo cha ununuzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas), baada ya kudai kubaini uwapo wa harufu ya ufisadi katika ununuzi wa taasisi hiyo.

Pamoja na mkuu huyo wa kitengo, Profesa Ndalichako pia aliagiza kuchunguzwa kwa watu wote watakaohusika katika sakata hilo.

Profesa Ndalichako alitoa uamuzi huo juzi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazoendelea chuoni hapo na kubaini matumizi mabaya ya fedha za umma.

Alisema kabla ya kwenda chuoni hapo, aliunda kamati ndogo ya kufuatilia tuhuma za ufisadi hususan kwenye masuala ya ununuzi na matokeo yalionyesha zina ukweli.

Aliongeza kuwa amebaini kuwa linapofika suala la ununuzi kwenye taasisi hiyo hakuna ushindani, badala yake kazi hizo anapewa mtu mmoja kupitia kampuni tatu tofauti. “Nimefanya uchunguzi wangu nimebaini kuna kampuni tatu ambazo zote zinamilikiwa na mtu mmoja ndizo zinazopata zabuni ya ununuzi katika chuo hiki, hakuna mchakato wa kushindanisha kampuni kama zinavyoagiza sheria za ununuzi serikalini,” alisema.

Profesa Ndalichako alibainisha hayo mbele ya menejimenti ya Muhas na kumpa maagizo nwenyekiti wa bodi ya chuo hicho, Mariam Mwaffisi kufanya uchunguzi zaidi akishirikiana na wajumbe wake wa bodi ili kuwanasa wote ambao kwa namna moja au nyingine wamehusika kupindisha utaratibu wa Serikali.

“Ninaagiza kusimamishwa kazi kwa mkuu huyo wa kitengo lakini si ajabu wapo wengine mapapa, mwenyekiti nitakukabidhi makabrasha yote niliyoyapata kutokana na uchunguzi wangu, fuatilieni hata kama ni makamu mkuu wa chuo, kama amehusika awajibishwe msimuogope mtu,” alisema

Pia, alitumia fursa hiyo kuagiza wakuu wa idara kuwa makini kwenye uagizaji wa vitu kulingana na mahitaji.