Mkuu wa mkoa aipasulia kampuni ya madini

Muktasari:

  • Katika ufungaji wa mgodi wa marumaru, watu watatu wakiwamo raia wawili wa China walikamatwa kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh92 milioni.

Ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu Serikali ilipoufunga mgodi wa mawe ya kutengenezea marumaru katika Kijiji cha Maseyu mkoani Morogoro, imewatahadharisha wachimbaji wapya kufanya shughuli zao kisheria.

Katika ufungaji wa mgodi wa marumaru, watu watatu wakiwamo raia wawili wa China walikamatwa kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh92 milioni.

Akizungumza jana, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe aliitaka kampuni ya madini ya Kiswila inayotarajia kuanza uchimbaji na upasuaji kokoto wilayani Mvomero kuzingatia sheria na taratibu za uchimbaji madini.

Kampuni hiyo ya madini inayotarajia kufungua mgodi mkubwa, pia imetakiwa kabla ya kuanza kazi ya uzalishaji ihakikishe uzalishaji wake unaweza kutosheleza mahitaji yaliyopo nchini.

Dk Kebwe alisema hayo alipotembelea eneo la mgodi huo uliopo Kijiji cha Melela kuangalia shughuli zitakazotarajiwa kufanywa na mgodi huo.

Mhandisi Petro Kingu ambaye pia ni mbia wa kampuni hiyo alisema shughuli za upasuaji mawe katika eneo hilo ulioanza miaka ya 1980, kokoto zilizotoka eneo hili ndizo zilizotumika katika ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Chalinze - Mlandizi hadi Dar es Salaam na Bwawa la Maji la Mindu lililopo Morogoro.