Friday, February 2, 2018

Mradi wa Mlimani City wawasha moto bungeni

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), jana imewasilisha ripoti ya shughuli zake iliyobeba mambo manne, ukiwamo mradi wa Mlimani City uliopo Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) na kulitaka Bunge limuombe Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuufanyia ukaguzi na kuwasilisha ripoti bungeni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka alieleza dosari za mradi huo, huku baadhi ya wabunge wakieleza namna walivyofanya kikao cha kamati eneo la Mlimani City, Januari 18 mwaka huu na kushuhudia mambo yasiyoeleweka.

Mbali na mradi wa Mlimani City, kamati hiyo ililitaka Bunge kuazimia kumuomba CAG kuchunguza ununuzi wa magari 777 uliofanywa na Jeshi la Polisi nchini kwa maelezo kuwa umejaa dosari.

Pia, iliishauri Serikali kufanya kila njia kuhakikisha fedha za umma Sh219 bilioni ilizowekezwa katika mradi wa Dege Eco Village uliopo Kigamboni unaotekelezwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) hazipotei na kuitaka kulipa madeni inayodaiwa na mifuko ya hifadhi za jamii.

Januari 18 mwaka huu, PAC iliutaka uongozi wa chuo hicho kurekebisha mkataba kati yake na Kampuni ya Mlimani Holding Limited (MHL) kutokana na upungufu uliojitokeza, huku ikihoji sababu ya mwekezaji huyo kuja na mtaji wa Sh150,000.

Jana, wakati akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, Kaboyoka alisema: “CAG afanye ukaguzi katika mchakato mzima wa mikataba yote inayohusu mradi huo na kuwasilisha taarifa ya ukaguzi huo bungeni.”

Alizitaja dosari walizobaini katika mradi huo ni kukiukwa kwa sheria ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inayosema ili kibali cha uwekezaji kitolewe, lazima mwekezaji alete ushahidi wa kuwa na mtaji wa kutosha.

Alisema mtaji wa Dola75 za Marekani (Sh150,000) ulioonyeshwa katika hesabu za MHL ni kinyume cha sheria ya TIC.

Kaboyoka alisema Turnstar Holding Limited ni miongoni mwa wanahisa wa MHL anayemiliki hisa moja na kwamba kampuni hiyo ya Turnstar imetoa mikopo kwa MHL wa Dola 49 milioni za Marekani.

“Kamati inapata shaka kuhusu nia ya mbia huyo kwa kuwa MHL ana hisa 900 ambazo hazijanunuliwa, hivyo angeweza kununua badala ya kukopesha(mbia),” alisema Kaboyoka.

Alifafanua kuwa kwa zaidi ya miaka 13 tangu mkataba uingiwe, mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tatu yenye vyumba 100 bado haujaanza kinyume na makubaliano.

Alibainisha kuwa kumekuwa na ukiukwaji wa malipo ya pango la ardhi ya UDSM na kwamba MHL amekuwa akipangisha wapangaji wengine bila kupata kibali cha chuo hicho, hivyo kusababisha kukosa mapato.

“Kamati hairidhishwi na mazungumzo yanayoendelea kati ya Chuo Kikuu na MHL,” alisema Kaboyoka.

Wabunge wanena

Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Allan Kiula alisema walipotembelea mradi huo waligundua maeneo ambayo walikubaliana kimkataba, hayajaendelezwa.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Catherine Ruge alisema mradi wa Mlimani City una maajabu saba ambayo unaweza kuyaona nchini pekee.

“Kinachonishangaza, UDSM ndiyo inazalisha wanasheria wabobezi lakini hawakuona upungufu hadi CAG alivyoanza uchunguzi,” alisema.

Ununuzi magari ya Polisi

Kuhusu ununuzi wa magari 777 uliofanywa na Jeshi la Polisi, alisema ulifanyika bila kuwa na mkataba na kuleta mkanganyiko. Alisema magari yaliyopokewa ni 181, ambayo hayajapokewa ni 596 huku fedha ambayo imelipwa hadi sasa ni asilimia 20 tu.

Kaboyoka alibainisha kuwa magari hayo yalipangwa kununuliwa kwa mkopo wa Benki ya Exim ya India, lakini mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Ashok Leyland uliingiwa Septemba 5, 2017 wakati mkataba wa mkopo kati ya Serikali na benki hiyo ulisainiwa Juni 19, 2015.

Mradi wa Dege Kigamboni

Kuhusu mradi wa Dege Kigamboni, Kaboyoka alisema umekwama kukamilika kwa wakati na unakabiliwa na changamoto.

“Kutokamilika kwa mradi huo kunaweza kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma,” alisema na kutaka Serikali iufanyie tathmini mradi huo.

Madeni mifuko ya hifadhi ya jamii

Kuhusu mifuko ya hifadhi za jamii, Kaboyoka alisema hadi hadi kufikia Juni 30, 2016 Serikali ilikuwa inadaiwa Sh1.6 trilioni katika mifuko mbalimbali.

-->