Mwakyembe aitaka TCRA kutoa mwongozo wa ving’amuzi

Muktasari:

  • Amesema kampuni zilipewa leseni ya kuonyesha chaneli za kulipia lakini zikaingilia soko la wenzao kinyume cha utaratibu wa leseni zao.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kutoa mwongozo utakaowezesha kampuni za ving'amuzi za Azam, DSTV na Zuku kurusha maudhui ya chaneli za ndani.

Amesema kampuni hizo zimelazimika kuondoa chaneli za ndani katika ving'amuzi vyake baada ya kukiuka masharti ya leseni zao.

Dk Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo Agosti 14 wakati akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Idara Habari Maelezo, jijini Dar es Salaam.

Amesema kampuni zilipewa leseni ya kuonyesha chaneli za kulipia lakini zikaingilia soko la wenzao kinyume cha utaratibu wa leseni zao.

"Inaelekea hawa wenzetu wanapenda kurusha haya maudhui ya chaneli za ndani, hivyo TCRA itoe mwongozo wa  nini wafanye ili kuendelea kutoa huduma,” amesema.

"Kama wamevutiwa na soko la kurusha maudhui haya basi wasifanye mbinu za chini chini badala yake wafuate utaratibu," amesema Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe amesisitiza kuwa kampuni hizo zilivunja masharti ya leseni zao lakini Serikali iliwavumilia kwa kuheshimu utawala wa sheria.