Mwalimu amuua mkewe, ajinyonga wakigombea nyumba

Muktasari:

Mwalimu huyo alichukua uamuzi wa kumuua mkewe na kisha yeye kujiua baada ya mkewe kumkatalia kuiuza nyumba yao.


Morogoro. Mwalimu wa shule ya  Msingi Duthumi wilayani Morogoro Respicius Salehe (46) amemuua mke wake, Scrinda Andrew (42) kwa kumjeruhi na kitu chenye ncha kali kichwani na baadaye naye kujiua kwa kujinyonga chanzo kikiwa ni ugomvi uliotokana na kuuza nyumba yao.

Akizungumzia tukio hilo leo Februari 19  kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Ulrich Matei amesema tukio hilo limetokea Februari 17  mchana maeneo ya Lukobe.

Kamanda Matei amesema  kuwa mwili wa mwalimu huyo umekutwa ukining’inia  kwenye mti wa mwembe baada ya kujinyonga kwa kutumia kitenge siku moja baada ya kumuua mke wake.

Amesema kuwa ugomvi uliosababisha mauaji ya wanandoa hao ulitokea baada ya mke kumpinga mume wake aliyetaka kuuza nyumba yao iliyopo Lukobe manispaa ya Morogoro.

Hata hivyo Kamanda Matei amesema  kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kubaini sababu zaidi ya mauaji ya wanandoa hao na kwamba marehemu wote wameshazikwa.

Katika tukio jingine mtu mmoja anayetuhumiwa kuwa mwizi maarufu wa ng’ombe, Dominick Chilala ameuawa kwa kupigwa na risasi shingoni na mguuni wakati akijaribu kuiba ng’ombe kwenye zizi.

Tukio hilo limetokea  Februari 15  mchana maeneo ya Mkambarani  ambapo ng’ombe hao walikuwa ni mali ya Zephania Masawe ambaye alifyatua risasi kutoka kwenye bunduki aina ya shortgun na kumuua mtu huyo.

Kamanda Matei alisema kuwa kabla ya kuuawa mtu huyo alikuwa akitafutwa na jeshi la polisi kwa muda mrefu kwa tuhuma za kuhusika kwenye matukio ya wizi wa mifugo.

Alitaja baadhi ya matukio aliyokuwa akituhumiwa kuhusika nayo mtu huyo ni pamoja na tukio la wizi wa ngo’mbe walioibwa kwenye maonyesho ya kilimo ya Nanenane mwaka jana pamoja na wizi wa ng’ombe 22 wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua).

Alisema kuwa mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi wa kidaktari na tayari ndugu wameshakabidhiwa mwili huo kwa ajili ya mazishi.

Kufuatia matukio hayo Kamanda Matei alitoa wito kwa jamii kutokata tamaa na kupelekea kujitoa roho huku akiwataka wezi wa mifugo kuacha tabia hiyo kwa kuwa Morogoro si sehemu salama kwa wahalifu wa aina yoyote.